Rais Samia aweka jiwe la msingi upanuzi wa bandari ya Ujiji na Kibirizi

Rais Samia ameweka jiwe hilo la msingi leo Jumanne ya Oktoba 18, 2022 ikiwa ni katika kuhitimisha ziara yake mkoani humo ambapo kabla ya uzinduzi huo tayari amefanya...

0
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof Makame Mbarawa na viongozi wengine wakati akivuta kitambaa kuashiria uwekaji wa jiwe la Msingi mradi wa Ujenzi wa Makao Makuu ya Bandari za Ziwa Tanganyika (Kibirizi na Ujiji)

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi kwa ajili ya upanuzi wa bandari ndogo ya Ujiji na Kibirizi mkoani Kigoma.

Rais Samia ameweka jiwe hilo la msingi leo Jumanne ya Oktoba 18, 2022 ikiwa ni katika kuhitimisha ziara yake mkoani humo ambapo kabla ya uzinduzi huo tayari amefanya shughuli mbalimbali ikiwemo uzimaji wa majenereta baada ya Kigoma kuunganishwa na gridi ya Taifa.

Wakati akiingia bandari ya Kibirizi Rais Samia alionekana kutofurahishwa na sura aliyoiona nje ikiwemo barabara na wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika eneo hilo.

Amesema tayari ameteta na Waziri wa Ujenzi ili waisaidie Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) kujenga barabara inayoingia bandarini hapo.

Lakini pia sikupendezwa na vibanda nilivyoviona, kwa maana hiyo kuna haja ya mwongozo wa mkoa na wilaya hii, kuliangalia hilo eneo, kushirikiana na wataalamu kupata ramani itakayopendezesha eneo hili la biashara ya kuingia bandarini.

“Ombi langu kwenu wafanyabiashara wa eneo hili, tukubaliane na yale yakayokuja kufanyika, kwa sababu maendeleo ni kuharibu kwanza, lazima tubomoe vibanda vilivyopo, tufanye ramani mpya halafu soko litakalokubaliwa lijengwe, halafu wale walioondoshwa warudishwe,” amesema Samia.

Amesema wakati akienda kutafuta fedha ya kujenga eneo hilo pia wao wakae na umoja wao wa wafanyabiashara wakubaliane jinsi eneo hilo litavyotengenezwa ili mtu atakapotoka bandarini akute wafanyabiashara wakiwa katika maeneo mazuri na wanafanya biashara nzuri.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), upanuzi wa bandari ya Kibirizi na Ujiji ni sehemu ya mradi mkubwa unaohusisha bandari tatu ikiwemo hiyo ya Kibirizi, Ujiji na bandari kuu ya Kigoma ambako jengo jipya litajengwa.

Katika bandari ya Kibirizi yanajengwa majengo ya kupokea mizigo, abiria na ofisi pamoja na ujenzi wa gati.

Kwa upande wa Ujiji litajengwa jengo la kupokea abiria, kantini huku mradi mzima ukigharimu bilioni 32, mradi ambao ulianza mwaka 2019.

Hadi sasa mradi wa Kibirizi umefikia asilimia 69.5 na upande wa Ujiji mradi umefika asilimia 61 huku majengo yakiwa yameshakamilika katika maeneo yote na yanatumika.

Mbali na kuweka jiwe hilo la msingi ametaka uongozi wa mkoa huo kushirikiana na wataalamu kuandaa ramani itakayopendezesha eneo la kuingia bandarini ikiwemo kujenga miundombinu mipya ya wafanyabiashara.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted