EAC kuzungumzia amani ya DRC, yapanga kuzungumza na Tshisekedi                       

Taarifa ya EAC kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Dk Peter Mathuki anatarajiwa kuungana na mwezeshaji wa mchakato wa amani mashariki mwa DRC,...

0

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imepanga kuzungumza na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Félix Tshisekedi mjini Kinshasa kuhusu amani mashariki ya nchi hiyo.

Taarifa ya EAC kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Dk Peter Mathuki anatarajiwa kuungana na mwezeshaji wa mchakato wa amani mashariki mwa DRC, Rais mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta katika kazi hiyo ya siku mbili iliyoanza jana.

Washauri wa Mwenyekiti wa Mkutano wa wakuu wa nchi za EAC na Rais wa Burundi, Évariste Ndayishimiye pia wamealikwa kwenye mazungumzo hayo.

Mazungumzo ya DRC chini ya mchakato wa amani unaoongozwa na EAC yametiwa nguvu tena ili kuwashirikisha viongozi na wadau wote wa jumuiya hiyo katika kutafuta suluhu kutokana na hali tete ya usalama iliyopo nchini humo.

Mkutano huo unafanyika wiki moja baada ya mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa EAC kufanya mkutano uliohusu mchakato wa amani mashariki mwa DRC, katika Jiji la Shamar El Sheikh nchini Misri wakati mkutano wa Mkakati wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) ukiendelea.

Mkutano huo ulioongozwa na Rais Ndayishimiye ulithibitisha kwamba nchi zote saba wanachama wa EAC zitashiriki kikamilifu katika mchakato huo, huku kila mkuu wa Nchi akimtuma mshauri kusaidia mwezeshaji wa mchakato wa amani wa EAC.

Wakuu wa nchi kutoka Jamhuri ya Uganda, Kenya, Rwanda na Tanzania walisisitiza dhamira yao ya kuchangia Mfuko Maalumu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ajili ya utekelezaji wa mchakato wa amani na kuzitaka nchi Wanachama zote kuunga mkono mpango huo kwa uendelevu.

Hivi sasa, Umoja wa Afrika na Mkutano wa Kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) umechangia Mfuko Maalumu wa EAC kwa ajili ya utekelezaji wa mchakato wa amani.

EAC inatarajia kufanya Mkutano wa Amani ifikapo mwishoni mwa mwaka huu huku moja ya mambo katika ajenda ikiwa ni kufikiria uwezekano wa kuoanisha mchakato wa amani unaoongozwa na EAC na Mchakato wa Luanda, ambao una mamlaka na majukumu ya ziada.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted