Mtoto afariki dunia kwa kuangukiwa na ukuta

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamisi Issah, alisema tukio hilo limetokea Novemba 10, majira ya saa 10 jioni wakati mtoto aliporudi shule na kukuta mlango wa nyumbani...

0

Mtoto Esanto Mtewa (7) wa Kijiji cha Utilili, wilayani Ludewa mkoani Njombe, amefariki dunia baada ya kuangukiwa na ukuta wa boma la nyumba wakati akijikinga mvua.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamisi Issah, alisema tukio hilo limetokea Novemba 10, majira ya saa 10 jioni wakati mtoto aliporudi shule na kukuta mlango wa nyumbani kwao umefungwa na kuamua kujikinga kwenye boma hilo wakati mvua ikinyesha.

“Kulikuwa na mvua kubwa sana iliyoambatana na upepo, mtoto huyu alirudi kutoka shule na nyumbani kulikuwa hakuna watu akajisitiri kwenye ukuta wa pagale ambalo ni jirani na nyumba yao,” alisema Kamanda Issah.

Alisema pagale hilo lilipigwa na upepo wa mvua na kubomoa ukuta uliomwangukia mtoto.

Kamanda alisema, wazazi waliporudi walilala mpaka asubuhi bila ya kuangalia mtoto wao yuko wapi na walipomtafuta baadaye waliona ukuta umeanguka huku mguu wa mtoto ukiwa umetokeza na kubaini ni mtoto wao.

Kamanda Issah alisema huo ni uzembe wa wazazi kulala bila kujua mtoto alipo.

“Kwa hiyo tunawasihi wazazi wengine ambao mnaweza mkaingia ndani mkalala bila ya kujua watoto wamelalaje hii ni namna fulani ya kauzembe, wazazi msiwe na hiyo hali ya kuwasahau watoto, kwetu sisi huu uzembe tunasema ni ukatili kwa hiyo tunawaomba msiwe na hiyo hali ya ukatili muwalinde watoto,” alisema.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted