Makalla:Hakuna mgao wa ya Maji Dar

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Amos Makalla ametangaza kuanzia sasa hakuna mgao wa maji ndani ya mkoa huo na kuitaka Mamlaka ya Majisafi na Mazingira...

0

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Amos Makalla ametangaza kuanzia sasa hakuna mgao wa maji ndani ya mkoa huo na kuitaka Mamlaka ya Majisafi na Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) kuelekeza nguvu kuimarisha miundombinu na miradi mikubwa ikiwemo Mabwepande.

Oktoba 24, 2022, RC Makalla alitangaza kuwepo kwa mgawo huo baada ya kutembelea vyanzo vya kuzalisha maji vya Ruvu Chini na Ruvu Juu na kujionea upungufu katika uzalishaji wa maji kulikosababishwa na ukame.

Leo Ijumaa, Novemba 25, 2022, mara baada ya kutembelea chanzo cha maji Ruvu Chini, RC Makalla ametangaza kuisha hali hiyo baada ya kuona ujazo wake umerejea kwenye hali yake ya kawaida kufuatia mvua zilizonyesha siku za hivi karibuni.

“Maji yamerejea katika ujazo wake wa kawaida na zaidi na kama mnavyojua vyanzo vya maji vinavyotegemewa ni Ruvu Juu inayochangia lita196 milioni na hapa Ruvu Chini inachangia maji lita 270 milioni na kufanya jumla kuwa lita za ujazo 466 milioni na sasa tuna maji ya kutosha,” amesema

Amesema walipokuja kutembelea mara ya kwanza walikuta maji yamekauka kabisa hivyo walianza kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwatoa watu wote wanaofanya shughuli zao karibu na vyanzo vya maji kuanzia milima ya Urugulu mkoani Morogoro hadi Pwani.

Aidha, amesema Dawasa walichukua hatua ya kufukua visima 20 katika mkoa wa Dar es Salaam na kufanya kufikia idadi ya visima 162 na katika kipindi chote cha ukame vilisaidia kupunguza changamoto ya maji.

Pia amesema anashukuru jitihada zilizofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kutoa Sh24 bilioni kwa ajili ya mradi wa Kigamboni unaozalisha lita za ujazo 70 milioni ilisaidia kupunguza makali ya mgao wa huduma hiyo.

“Visima 162 vinachangia lita 33.9 milioni na Sasa tunayo maji ya kutosha kwa mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, nawapongeza Dawasa kwa jitihada zao waliochukua katika kipindi kigumu na nawatangazia hakuna tena mgao wa maji,” amesema

Aidha, aliwashukuru wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam kwa kuwa wavumilivu katika kipindi chote cha hali ngumu ya mgao wa maji walichopitia huku Serikali ikifanya jitihada za kila namna kutatua tatizo hilo.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema ni vigumu kuelezea hali waliyopitia na kudai wakati wa mgao wa huduma hiyo waliokuwa kwenye wakati mgumu.

“Wateja wote wa kwetu na kama hawapati maji wanatafuta majibu kulikuwa kipindi kigumu kama cha wiki tatu hivi, Lakini nieashukuru viongozi wa dini kilicchofanyika kama miujiza mvua zimengesha na maji yame jaa,” amesema

Amesema kutokana na hatua walizochukua mkoa wa Dar es Salaam na Pwani wanamaji ya kutosha zaidi ya mahitaji yake.

“Ukichukua maji ya Ruvu juu,Ruvu Chini,Wami na kigamboni ni kama Jumla ya  lita 590 milioni  wakati mikoa hiyo mahitaji yake ni Lita 544 milioni,” amesema

Hata hivyo, amekiri changamoto ya miundombinu bado ni tatizo linalowaumiza kichwa huku wakiishukuru Serikali kwa kuendelea kuwapa fedha kwa ajili ya ushughukia hilo.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted