Rais Samia:Siridhishwi na kasi ya uendeshaji wa miradi ya UWT

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kutoridhishwa na kasi ya kujiunga kwa wanachama wa Jumuiya ya wanawake wa chama hicho (UWT) na uendeshaji...

0

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kutoridhishwa na kasi ya kujiunga kwa wanachama wa Jumuiya ya wanawake wa chama hicho (UWT) na uendeshaji wa miradi yake ya kiuchumi.

Rais Samia ameyasema hayo leo Novemba 28, 2022 wakati akizungumza kwenye mkutano mkuu wa uchanguzi wa UWT jijini Dodoma, ambapo amesema kuwa kuanzia mwaka 2017 hadi 2022 Jumuiya hiyo imeingiza wanachama wapya 86,288 ambao amesema sio idadi nzuri kwao.

“Ukichukua idadi hiyo ukiigawa kwa mikoa 32 na kujua mikoa mengine ni midogo sana kama ile ya Zanzibar unapata wanachama 2697 tu sasa hii sio kazi nzuri sana,” amesema.

Samia amesema jumuiya hiyo ilikuwa na muda wa kutosha wa kuongeza wanachama wengi zaidi wakati nchi ilipokuwa haina hekaheka za kisiasa na kutumia makongamano kujitangaza.

Akizungumzia upande wa miradi ya kiuchumi, Rais Samia amesema miradi hiyo haijaipa UWT nguvu kubwa ya kiuchumi hivyo kuwa na tabia ya kushika na kuacha miradi hiyo.

Amesema miradi inayoendeshwa na Jumuiya hiyo mingi ni ya vibanda, mashine za kusaga na mingine midogo ambayo haijaipa nguvu kiuchumi UWT.

“Wito wangu kwa Jumuiya ni kwenda kufanya miradi mikubwa itakayoipa Jumuiya nguvu ya kiuchumi,” amesema Samia.

Rais Samia amesema aliona wakati wa maandalizi ya kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi huo namna Kamati mbalimbali zilifatwa kuangalia upatikanaji wa fedha.

“Baadae nikasema msisumbuke kwa hiyo chama na mimi tukatoa fedha mambo yakaenda, hii inaonesha kuwa miradi tuliyonayo bado haijawa miradi ya kutupa nguvu ya kiuchumi kwenye Jumuiya,” amesema Samia.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amesema Jumuiya ya Wanawake ya chama hicho (UWT) imeanza kujisahau kwa kuacha kuwa viongozi wa jumuiya na chama na badala yake kuwa viongozi wa watu.

Amesema jumuiya hiyo ina nguvu sana lakini nafikiri kuna mahali kuna kujisahau kwa kutokaa katika nafasi zao.

“Kuna mahali tunaanza kujisahau, tunaacha kuwa viongozi wa jumuiya ya wanawake, viongozi wa jumuiya na chama tunakuwa viongozi wa watu. Hilo jambo linatengeneza changamoto kubwa ya uimara wa UWT na nguzo muhimu ya wanawake,” amesema.

Amesema ni lazima kutambua chama ni kikubwa kuliko mtu yoyote na kwamba ni lazima wasimame katika nafasi zao na kurudi kwenye misingi ya chama ya chama chao.

Naye Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana amewataka wanawake hao kushikamana na kuwa kitu kimoja wakati wote kwasababu nguvu ya chama chao ni umoja na mshikamano.

“Jumuiya ya wanawake inatarajia kuwa jumuiya ambayo inatetea maslahi makubwa na mpana ya wanawake wote nchini. Ni muhimu mkaelewa sera za chama chetu mtakaochaguliwa,” amesema.

Awali, Katibu Mkuu wa umoja huo, Dk Philis Nyimbi alisema idadi ya wajumbe wote waliowa wakitakiwa ni 830 lakini waliokuwa ukumbini walikuwa 802 hivyo akidi iliyotakiwa ilikuwa imefikiwa.

Viongozi waliohudhuria ni pamoja na viongozi wastaafu Makamu wa CCM Bara, Philip Mangula, Mwenyekiti mstaafu wa UWT, Sophia Simba na Spika mstaafu Anne Makinda.

Wengine ni wawakilishi wa vyama vya siasa kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Frelimo (Msumbiji), Zanu PF (Zimbabwe) na ANC (Afrika Kusini).

Pamoja na mambo mengine, mkutano huo utafanya uchaguzi wa viongozi mbalimbali wakiwemo wa nafasi ya uenyekiti ambapo wagombea watano wanachuana vikali.

Wagombea waliopitishwa na Halmashauri Kuu ni, Gaudentia Kabaka (anayetetea nafasi yake), Kate Kamba, Dk Wemael Chamshama, Mariam Lulinda na Mary Chatanda huku mchuano mkali ukionekana kwa Gaudentia Kabaka, Kamba na Mary Chatanda.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted