Ucheleweshaji wa tume huru wamtia wasiwasi Prof Lipumba

Chama cha Wananchi (CUF) nchini Tanzania, kimemuomba Rais wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan, atimize ahadi yake ya kujenga maridhiano na kuimarisha demokrasia ya vyama vingi, kwa kuhakikisha...

0

Chama cha Wananchi (CUF) nchini Tanzania, kimemuomba Rais wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan, atimize ahadi yake ya kujenga maridhiano na kuimarisha demokrasia ya vyama vingi, kwa kuhakikisha tume huru ya uchaguzi inapatikana kabla ya chaguzi zijazo. 

Akizungumza na waandishi wa habari, jana Jumatatu, 28 Novemba 2022, Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema upatikanaji wa tume hiyo ni muhimu katika kufikia lengo la kuwa na siasa za kistaarabu pamoja na maamuzi ya wananchi kuheshimiwa.

“Nilikuwa navutiwa na kauli ya Rais Samia pamoja na sera yake ya maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na ujenzi mpya wa taifa. Ni muhimu atembee kwenye maneno yake kivitendo, tuelezwe mpango kazi wa kupata tume huru ya uchaguzi,” amesema Prof. Lipumba.

Prof. Lipumba amesema anatiwa shaka na hatua ya Serikali kutoweka mpango mkakati wa kupatikana kwa tume hiyo, licha ya Kikosi Kazi Cha Rais Samia kuwasilisha ripoti yake iliyobeba maoni ya wadau kuhusu maboresho ya demokrasia ya vyama vingi.

“Mchakato wa katiba mpya ni muhimu lakini uchagu,I hauwezi kuahirishwa lazima tupate tume huru ya uchaguzi ambayo itaweza simamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2025. Napata wasiwasu mpaka Sasa hivi sijasikia kama Baraza la mawaziri limekutana kujadili mpango kazi wa kutekeleza haha mambo muhimu ya kupata Katiba mpya na tume huru ya uchaguzi,” amesema Prof. Lipumba.

Mwenyekiti huyo wa CUF amesema “muda unakwenda maamuzi yasipofanyika tunaweza tukajikuta tunaingia 2024 kwenye uchaguzi yanarejea yaliyotokea 2019 wagombea wengi walienguliwa hawakupata fursa ya kuweza kushiriki uchaguzi mkuu.”

Katika hatua nyingine, Prof. Lipumba ameiomba Serikali ya Rais Samia iweke wazi mpango kazi wa kutekeleza mapendekezo ya wadau yaliyokusanywa na kikosi kazi, ikiwemo ya ukamilishaji mchakato wa kupata katiba mpya, kufunguliwa mikutano ya hadhara, ushiriki wa wanawake katika siasa, maboresho dhidi ya Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria za uchaguzi.

Katika hatua nyingine, Prof. Lipumba amewataka wananchi kudai haki ya kufanya siasa na demokrasia ya kweli kwa kuwa ndiyo msingi wa maendeleo yao.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted