BoT:Kuna ongezeko la udanganyifu wa miamala ya kifedha

BoT imesema matukio mengi ya taarifa hizo yanahusisha kiasi kikubwa cha pesa kinachodaiwa kuletwa kwa ajili ya ufadhili wa mradi au matumizi binafsi.

0

Benki Kuu ya Tanzania imebaini kuongezeka kwa udanganyifu miamala ya kifedha nchini humo unaohusisha mwananchi kupokea taarifa(hati au barua pepe) inayodai kuwa ni uthibitisho wa malipo kupitia SWIFT au mifumo mingine ya uhamishaji fedha.

Taarifa iliyotolewa leo na benki hiyo imeeleza kuwa mpokeaji anafahamishwa kuwa fedha zimeingizwa kwenye benki au akaunti katika taasisi ya fedha nchini Tanzania wakati mwingine, mpokeaji fedha anaelekezwa kulipa kiasi fulani cha fedha kuwezesha kupata fedha hizo nyingi.

BoT imesema matukio mengi ya taarifa hizo yanahusisha kiasi kikubwa cha pesa kinachodaiwa kuletwa kwa ajili ya ufadhili wa mradi au matumizi binafsi.

Hivyo, Benki Kuu ya Tanzania imeutaarifu umma kwamba taarifa hizo ni za kughushi na za kubuni.

“Wananchi mnashauriwa kuwa waangalifu na kuacha kujihusisha na miamala hiyo ambayo kwa kawaida inalenga kuwatapeli fedha” imesema taarifa hiyo.

Aidha BoT imewataka wananchi kuzingatia kanuni bora za kufanya miamala ya fedha ili kuepuka upotevu wa fedha ambazo ni kuhakikisha usalama wa taarifa za fedha wakati wa kutoa taarifa binafsi mtandaoni (tovuti, mitandao ya kijamii), kupitia barua pepe au kwenye simu, kutojihusisha kujibu barua pepe, barua au simu zinazoahidi kupokea fedha kutoka kwa watu au kampuni wasizozifahamu vizuri na kuwa waangalifu wanapofanya malipo ya mtandaoni kwa kufanya uhakiki wa mshirika wa kibiashara (mtu au kampuni) kabla ya kutoa maelezo au kufanya malipo.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted