Mwili wa Mtanzania aliyefia Ukraine kurudishwa Tanzania kwa ajili ya maziko

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, nchini Tanzania, Dk Stergomena Tax  mtanzania huyo alikwenda nchini Urusi mwaka 2020 kwa ajili ya...

0

Serikali ya Tanzania imesema mwili wa Mtanzania aliyefariki dunia vitani nchini Ukraine, Nemes Tarimo umeondoka Urusi kuja nchini humo kwa ajili ya maziko.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, nchini Tanzania, Dk Stergomena Tax  mtanzania huyo alikwenda nchini Urusi mwaka 2020 kwa ajili ya masomo ya shahada ya uzamili katika fani ya biashara, lakini mwezi machi 2022 alipatikana na hatia ya uhalifu na kuhudukumiwa kifungo cha miaka 7.

Waziri huyo amesema wizara yake imepokea taarifa kutoka serikali ya Urusi kuwa akiwa gerezani, Tarimo alipewa nafasi ya kujiunga na kikundi cha kijeshi cha Urusi kiitwacho Wagner kwa ahadi ya kulipwa fedha na kuachiwa huru baada ya kumalizika kwa vita hiyo.

Mtanzania huyo alikubali kwenda vitani na umauti ukamkuta vitani oktoba 24, 2022.

“Ikumbukwe kwamba kwa mujibu wa Sheria zetu, Mtanzania yeyote haruhusiwi kujiunga na jeshi la nchi yoyote isipokuwa Jeshi la Tanzania. Hivyo, nitoe rai kwa Watanzania wote kuhakikisha wanazingatia sheria za nchi yetu, kanuni na taratibu zilizopo.

“Napenda kuuhakikishia umma pamoja na diaspora wa Kitanzania ikiwemo wanafunzi walioko masomoni nchini Urusi kuwa Serikali kupitia ubalozi wake uliopo Urusi itaendelea kuwapa ushirikiano na kuhakikisha Watanzania hao wako salama wakati wote,” amesema Dk Tax.

Mwili wa Bwana Tarimo umeondoka Urusi kurejeshwa Tanzania kwa ajili ya maziko.

Juma lililopita taarifa za kifo cha Raia wa Tanzania, Nemes Tarimo, zilisambaa kwenye mitandao pamoja na video ikionesha akiwa anaagwa kwa heshima na vikosi vya jeshi nchini Urusi.

Baadaye familia ya Nemes Tarimo ilithibitisha kutokea kwa kifo hicho na kuwa wanasubiri mwili wa mpendwa wao kwa ajili ya Maziko.

Kwa mujibu wa famili ya Tarimo, mwili ukishapokelewa ataagwa jijini Dar es salaam, kisha kusafirishwa hadi nyanda za juu kusini mwa Tanzania kwa ajili ya Maziko. 

Taarifa ya kwanza kutoka kwenye familia hiyo walisema hawakuwa wanajua kuwa mtoto wao alikuwa amefungwa na hawakujua pia kuwa alijiunga na kikundi hicho cha kijeshi cha Urusi na kwenda vitani Ukraine. Walisema walichokuwa wanakijua ni kwamba alikuwa Urusi kwa ajili ya masomo.

Hata hivyo walipata taarifa kutoka marafiki wa karibu Nesemi kuhusu habari hizo pamoja na kifo chake mwishoni mwa mwezi Desemba, kabla ya kuarifiwa na Ubalozi wa Tanzania huko Moscow.

Nemes si mwafrika wa kwanza kufariki  akiwa anapigana vita kwenye jeshi la Urusi lakini hivi karibuni Raia wa Zambia, Lemekhani Nyirenda, 23, alifariki nchini Ukraine akiipigania Urusi, naye awali alikuwa akitumikia kifungo kinachohusiana na dawa za kulevya nchini Urusi lakini aliachiliwa na kupelekwa mstari wa mbele nchini Ukraine.Alifariki tangu mwezi Septemba, mwaka jana lakini familia yake ilichelewa kupata taarifa na mwili wake ulirudishwa nchini Zambia mwezi Desemba

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted