KUMBUKUMBU:Miaka miwili tangu kutokea kwa kifo cha Maalim Seif, gwiji wa siasa za Tanzania

Maalim Seif amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 76, huku akiwa ametumikia nyadhfa mbalimbali Serikalini lakini hadi umauti unamfika alikuwa makamu wa kwanza wa rais wa SMZ...

0

Tarehe na mwezi kama wa leo, Tanzania ilimpoteza gwiji wa medani za siasa Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye alifariki wakati akitibiwa jijini Dar es salaam.

“Ndugu wananchi wa Zanzibar na Watanzania kwa ujumla, kwa masikitiko makubwa nakujulisheni leo tarehe 17 Februari, 2021, majira ya saa tano asubuhi, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amefariki dunia.”

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi akitangaza kifo cha Maalim Seif, kilichotokea miaka miwili iliopita katika hospitali ya taifa Muhimbili, Dar es Salaam.

Maalim Seif amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 76, huku akiwa ametumikia nyadhfa mbalimbali Serikalini lakini hadi umauti unamfika alikuwa makamu wa kwanza wa rais wa SMZ kwa chini ya siku 100, akiwa sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoundwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2020.

Ameacha alama kubwa katika jukwaa la siasa, na wengi hutumia kivuli chake kama sehemu ya kujifunza kwa aliyoyafanya katika kupigania haki nchini.

Ni mwanasiasa ambaye aliisumbua sana Serikali na viongozi wake kwa kutokubali kushindwa pale ambapo aliona haki imekiukwa, hali iliyomfanya kusimamia misimamo yake bila kujali nini kingetokea mbele yake.

Nyuma ya Maalim Seif kulikua na wafuasi wengi waliomtazama kama shujaa kwenye mapinduzi ya jukwaa la kisiasa hususani visiwani Zanzibar, ambapo waweza sema alikubalika kwa zaidi ya asilimia 90.

Kifo chake kilihitimisha safari yake ya kisiasa ya mwanasiasa mashuhuri kuliko wote wa Zanzibar na kiongozi ambaye alizibeba siasa za upinzani katika visiwa hivyo katika muda wa miaka 30 iliyopita.

Mara zote amekuwa akichuliwa kama tishio kwa serikali zilizoko madarakani na amekuwa mhanga mkubwa wa kukamatwa ma polisi mara kwa mara

Kwa kipindi chote cha uhai wake amepambana na utawala wa CCM bila kuchoka, na bila kurudi nyuma. Amesimama kidete na kuhakikisha masilahi ya wananchi wa Zanzibar yanalindwa.

Matokeo ya jitihada zake katika siasa ni mengi, lakini kubwa zaidi ni kuundwa kwa nafasi ya makamu wawili wa rais wa Zanzibar.

Vilevile kuchochea mageuzi makubwa ndani ya Tanzania. Maalim amepambana na vigogo wakubwa kwenye chaguzi za kisiasa tangu mwaka 1995 (Salmin Amour), mwaka 2000 na 2005 (Amani Karume, mtoto wa rais wa kwanza wa Zanzibar Abeid Karume), mwaka 2010 na 2015 (Dk. Ali Mohammed Shein).

Maalim Seif ni nani haswaa?

Jina lake linatajawa sana kwenye ulingo wa siasa za Tanzania na hata nje ya Tanzania.Maalim Seif Shariff Hamad alizaliwa huko Nyali, Mtambwe kisiwani Pemba Oktoba 22,1943.

Aliwahi kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Zanzibar kuanzia mwaka 1984-1988, kisha akagombea mara kadhaa Urais wa nchi bila mafanikio licha ya kuwa alikua akipata kura nyingi Mara mbili alipata kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Alipataslimu yake ya msingi katika skuli ya msingi Uondwe mwaka 1950, na baadaye alijiunga na elimu ya sekondari katika skuli ya watoto wa kiume ya Wete Pemba 1952.Baadaye aliendelea na elimu ya sekondari katika skuli ya King George na kuhitimu kidato cha sita mwaka 1963, ambapo baadaye kati ya mwaka 1972 na 1975 alihitimu Chuo Kikuu cha Dar es salaam na kutunukiwa shahada ya kwanza ya Sayansi ya Siasa (Political Science).

Kabla ya kujiunga na siasa Maalim Seif aliwahi kuwa mwalimu ambapo alifanikiwa kufundisha katika skuli mbalimbali za Unguja na Pemba zikiwemo Fidel Castro na Lumumba. 

Baadaye Maalim Seif alianza kuingia katika masuala ya siasa ambapo mwaka 1977 aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni na Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi Mwaka 1977 hadi 1987, alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na kuwa Mjumbe wa Kamati kuu ya chama hicho.

ZIFF chief guest, 1st vice president, Maalim Seif Sharif at ZIFF 2013

Mwaka 1982 hadi 1987 alikuwa Mkuu wa Idara ya Uchumi na Mipango ya Chama cha Mapinduzi na 1984  aliteuliwa kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hadi mwaka 1988.

Baada hapo, misukosuko mikubwa ya kisiasa ilianza kumkumba ambapo Januari 1988 alipoteza nafasi ya Uwaziri Kiongozi na Ujumbe wa Baraza la Uwakilishi baada ya aliyekuwa Rais wa Zanzibar,Idrisa Abdulwakil kutangaza kulivunja Baraza la Mwaziri. 

Mei 1988, Maalim Seif alitoka katika chama cha CCM.

Mwaka 1992 Maalim Seif alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama cha CUF.

Alidumu ndani ya chama cha CUF kwa muda mrefu tangu alipokiahama chama cha CCM, lakini migogoro ndani ya chama hicho ilimfanya Maalim Seif kubadili njia.

Machi 18,2019  alitangaza kujiunga na chama cha ACT Wazalendo chama ambacho wakati huo ndo kilianza kukita mizizi yake kutokana na uchanga wake. 

Maamuzi hayo yalifanywa muda mchache baada ya kesi  iliyokuwa mahakamani kuishia kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa chama cha CUF.

Hamad alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa ACT Wazalendo, nafasi aliyopewa kando ya kiongozi wa kitaifa wa chama hicho Zitto Kabwe.

 Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 alirudia nafasi yake ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar katika serikali ya umoja wa taifa aliyokuwanayo .

Seif Sharif Hamad alifariki tarehe 17 Februari 2021 katika hospitali ya taifa ya Muhimbili baada ya kupatikana na Virusi vya Corona yeye pamoja na mke wake.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted