Dkt. Mpango atoa wito wa ushirikiano kwa nchi Zisizofungamana na Upande Wowote

Makamu wa Rais amesema hayo katika mji wa Baku nchini Azerbaijan, alipokuwa akihutubia mkutano wa nchi Zisizofungamana na Upande Wowote, mkutano uliolenga kujadili namna ya kukabiliana na athari...

0

Makamu wa Rais wa Tanzania,  Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa nchi zisizofungamana na Upande Wowote kuendelea kushirikiana katika kutumia fursa, kukuza biashara ya kimataifa na uwekezaji, kushirikishana mbinu bora na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.

Makamu wa Rais amesema hayo katika mji wa Baku nchini Azerbaijan, alipokuwa akihutubia mkutano wa nchi Zisizofungamana na Upande Wowote, mkutano uliolenga kujadili namna ya kukabiliana na athari za UVIKO – 19.

Amesema janga la UVIKO – 19 limetoa somo la kutotegemea msaada wakati wote, hivyo inapaswa nchi wanachama kuwekeza katika tafiti na maendeleo kwa ajili ya kutatua changamoto za ndani ya nchi ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa chanjo, vifaa tiba, vitendanishi na bidhaa nyinginezo za kuokoa maisha ya wananchi.

Dkt. Mpango pia ametoa wito wa kuhakikisha nchi hizo zinaimarisha uwezo katika ufuatiliaji, ili kutambua kwa wakati na kuzuia magonjwa ya kuambukiza.

Akitoa uzoefu wa Tanzania katika kukabiliana na athari za UVIKO -19, Makamu wa Rais amesema serikali ilihamasisha utoaji chanjo na kusambaza chanjo kwa walengwa, hatua ambayo ilisaidia katika kudhibiti janga hilo, kuongeza miundombinu za kutolea huduma za afya pamoja na kuongeza watoa huduma, vifaa tiba na dawa muhimu.

Hatua nyingine ni pamoja na kutumia mkopo wa masharti nafuu chini ya dirisha la Rapid Credit Facility (RCF) kutoka Shirika la Fedha Duniani, ili kuongeza uwezo wa miundombinu katika elimu.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted