Rais Samia ahaidi mchakato wa Katiba kuanza hivi karibuni

Ametoa ahadi hiyo leo tarehe 8 Machi 2023, katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, yaliyofanyika mkoani Kilimanjaro, baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kumuomba marekebisho...

0

Rais Samia Suluhu Hassan amesema hivi karibuni Serikali yake itatangaza kamati itakayokuwa na jukumu la kusimamia ufufuaji mchakato wa marekebisho ya katiba, uliokwama tangu 2014. 

Ametoa ahadi hiyo leo tarehe 8 Machi 2023, katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, yaliyofanyika mkoani Kilimanjaro, baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kumuomba marekebisho hayo yakamilike kabla 2025.

“Nilikuwa nasema hivi, suala la katiba hakuna anayelikataa hata chama changu kimesema twende kwenye mabadiliko ya katiba, hakuna anayelikataa lakini mdogo wangu Aikael kasema juzi leo lifanyike, mambo ni mengi ndani ya nchi lakini niwaahidi si muda mrefu tutatangaza hiyo kamati kwa kushirikiana na vyama vya siasa ili waende wakaanze kazi,” amesema Rais Samia.

Katika hatua nyingine, Rais Samia ametumia madhimisho yaliyoandaliwa na Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), kuwataka wananchi bila kujali tofauti zao za itikadi za kisiasa na dini, kukomesha vitendo vya mmomonyoko wa maadili nchini.

“Suala la maadili ya vijana wetu haipendezi, haifurahishi na hakuna wa kumtupia lawama. Lawama ni kwamba jamii yetu ya Tanzania tulitetereka kwenye malezi na dini. Twendeni tukaangalie tulikokosea, wapi tulinde mila na desturi yetu. Kuna mengine ya kuletewa tukatae,” amesema Rais Samia.

Kuhusu haki za wanawake, Rais Samia amewataka wanawake wa Bawacha washirikiane na wanawake kutoka vyama vingine vya siasa, kupigania maslahi ya kundi hilo.

“Ile nguvu ya watu ya wanawake wa Chadema ikaunganishe kila chama tukamkomboe mwanamke wa Tanzania, tukakuze uchumi ili yale tunayolilia hapa yakatekelezwe. Mkianza kuweka mipaka sitafanya na yule sababu hana hili hana hili hatutafika,” amesema Rais Samia.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted