Wasoma Mita za maji nchini Tanzania wawekwa kikaangoni

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewaonya wasoma mita za maji nchini kuacha tabia ya kuwabambikia wananchi bili kubwa za maji kwani hatua hiyo inaichafua serikali jambo ambalo...

0

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewaonya wasoma mita za maji nchini kuacha tabia ya kuwabambikia wananchi bili kubwa za maji kwani hatua hiyo inaichafua serikali jambo ambalo halitovumilika.

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo tarehe 16 Machi 2023 wakati akizindua wiki ya maji iliyoenda sambamba na uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa usambazaji wa maji kati ya Makongo na mji wa Bagamoyo.

Pia ametoa muda wa siku 14 kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuwaunganishia maji wananchi wanaozunguka tenki kubwa la maji lililopo maeneo ya Tegeta jijini Dar es Salaam. 

Amesema kumekuwapo na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wa maeneo ya Hedari na Same kwamba wanabambikiwa bili kubwa za maji kama vile wana viwanda katika nyumba zao.

Amesema ubambikaji huo wa bili umekuwa ukiichafua serikali jambo ambalo kamwe viongozi wa Serikali na mamlaka husika hazitokubali.

“Nisisitize hakuna mtu anatozwa bili kubwa kama anakiwanda, viwango vya malipo vinafahamika, ni vizuri ni kuchangia huduma ila kama una kiwanda hicho ni kitu kingine,” amesema.

Ameitaka DAWASA kukamilisha michakato ya kununua mita za kisasa ili kila mwananchi alipie bili kulingana na maji anayotumia na kiwango cha bili ambacho anakiona.

“Hivyo wasoma mita wasitumie nafasi hiyo kuchafua serikali kwa kulazimisha bili, tukikugundua tutashughulika na wewe hapohapo,”amesema.

Pia ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa iwapo mamlaka zinazowaunganishia maji zinataka rushwa.

Amesema kwa kuwa gharama za kuunganisha maji kwa mara ya kwanza zinafahamika, wananchi nao watambue haki yao na pindi kutakapotokea urasimu katika uunganishiwaji wa maji watoe taarifa kwa mamlaka husika.

“Usikubali mtu yeyote awe mtumishi wa Dawasa au kiongozi, akuombe rushwa ya kuunganisha maji, hakuna rushwa utakayotoa maji kuja kwako, uunganisha ni wa gharama zilezile,” amesema.

Aidha, amesema mradi huo wa tenki la maji Tegeta jijini Dar es Salaam unatarajiwa kunufaisha wananchi 450,000 kutoka maeneo ya Chuo kikuu cha Dar es Salaam hadi Bagamoyo mjini.

Awali Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alitoa wito kwa wananchi kuvunja ukimya na kutoa taarifa kwa viongozi na mamlaka zinazohusika pindi wanapobambikiwa bili za maji na wasoma mita.

“Hatutokubali kumuona msoma mita akimbambikizia mwananchi bili ya maji, niwaombe wananchi Rais Samia Suluhu Hassan ametuamini sisi viongozi wenu hivyo sehemu ambayo unapata changamoto usikae kimya, sisi viongozi tupo, atakayekuzinga tutashughulika naye hata awe na mapembe kiasi gani,” amesema Aweso.

Aidha, amesema katika bajeti zilizopita, fedha za maji zilizotolewa kwa asilimia 50 hadi 60 lakini katika uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, fedha za wizara hiyo katika miradi ya maji zimetolewa kwa asilimia 90.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted