Mwili wa Membe kuzikwa Mei 16

Mwili wa aliyekuwa Waziri wa  Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe unatarajiwa kuhifadhiwa kwenye nyumba yake ya milele Mei 16, mwaka huu katika kijiji cha...

0

Mwili wa aliyekuwa Waziri wa  Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe unatarajiwa kuhifadhiwa kwenye nyumba yake ya milele Mei 16, mwaka huu katika kijiji cha Londo mkoani Lindi.

Membe aliyepata kuhudumu kwenye wadhifa wa waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete, alifariki dunia, asubuhi ya leo, 12 Mei 2023, katika hospitali ya Kairuki, iliyopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam.

Membe amefariki akiwa na umri wa  miaka 69, ambapo sababu ya kifo chake imetajwa kuwa ni changamoto ya kifua.

LAKINI JE BERNARD MEMBE NI NANI?

Bernard Membe ni mwanasiasa nguri na mwanadiplomasia mashuhuri nchini Tanzania na Afrika ambaye amewahi kuhudumu katika nafasi kadhaa nyeti serikalini ikiwemo Idara ya Usalama wa Taifa, waziri wa Mambo ya Nje pamoja na kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada.

Huyu  ni mtoto wa pili kuzaliwa kati ya watoto saba wa familia ya mzee Kamillius Antony Chitakile na Cecilia John Membe ambapo alizaliwa Novemba 9, 1953 huko katika kijiji cha Rombo, Kata ya Chiponda mkoani Lindi.

Membe ametumikia nafasi mbalimbali ikiwemo Kamanda wa Vijana wa Mkoa wa Lindi, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa, na Katibu wa Sekretarieti ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa Chama Cha Mapinduzi.

Amekuwa Mbunge wa Jimbo la Mtama kwa awamu tatu tofauti mpaka mwaka 2015, ambapo alichaguliwa kuwakilisha jimbo hilo kwa mara ya kwanza waka 2000.

Mwaka 2006 aliteuliwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, ambapo Oktoba 2006 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Nishati na Madini na kisha Januari 2007 akateuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa. 

Membe alihudumu katika nafasi hiyo hadi 2015, akiwa ni Mtanzania wa pili kushika wadhifa huo kwa miaka mingi mfululizo, akitanguliwa na Rais Kikwete ambaye alidumu katika wizara hiyo kwa miaka 10 mfululizo.

Akiwa katika wizara hiyo, Tanzania ilipata ugeni wa viongozi wakubwa duniani kama Rais George W. Bush  mwaka 2008 na Baraka Obama (2013) wote wa Marekani,.

Wengine ni  Xi Jinping wa China (2013) , Joachim Gauck wa Ujerumani  (2015), Jacob Zuma wa Afrika Kusini (2014) , Mwana Mfalme wa Malkia (2011) wa Uingereza, na Mwana wa Mfalme wa Japan mwaka 2014.

Baadhi ya nyadhifa ambazo Membe amewahi kushika tangu mwaka  2006 ni pamoja na  Mwenyekiti Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Afrika, Addis Ababa, Ethiopia, Mkuu wa waangalizi wa uchaguzi mkuu wa Zimbabwe kutoka Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Katibu wa Sekretarieti ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya CCM  pamoja na kuwa Mwenyekiti Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Madola (Commonwealth).

PANDA SHUKA ZA KISIASA ZA MEMBE

Februari 28, 2020 Membe  alifukuzwa uanachama wa CCM na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya kwa kile kilichotajwa kuwa na mwenendo usiofaa ndani ya chama hicho. 

Membe alijiunga na ACT-Wazalendo Julai 15, 2020 na kugombea Urais wa Tanzania kupitia chama hicho ambapo alipata akura 81,129 sawa na 0.5% ya kura zote.

MADAI YAKE YA BILIONI 9 

Hadi umauti unamfika Membe anamdai aliyekuwa akijiita mwanaharakati huru Cyprian Musiba kiasi cha shilingi bilioni 9 kama fidia kutokana na kile alichokiita kuchafuliwa jina lake na gazeti la Tanzanite, ambalo lilikua linamilikiwa na Musiba.

Membe alifungua kesi mahakamani akimshtaki Mkurugenzi wa gazeti hilo Cyprian Musiba ambapo baada ya kushinda shauri hilo mahakama ilimuamuru Musiba kulipa zaidi ya Sh9 bilioni kama fidia.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted