Tanzania yajidhatiti kujenga Satelaiti yake

Endapo mpango huo utakuwa dhahiri, Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi za Afrika zilizofanikiwa kupeleka kifaa hicho angani, ambazo  ni Algeria, Ethiopia, Kenya, Zimbabwe, Afrika Kusini, Morocco, Misri, Ghana...

0

Serikali ya Tanzania imesema imeanza mazungumzo juu ya ujenzi wa satelite ili kuendana na mapinduzi ya teknolojia duniani.

Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwa katika uzinduzi wa mradi wa minara ya kurusha matangazo ya Televisheni ardhini (DTT) inayomilikiwa na kampuni ya Azam Media Limited.

Endapo mpango huo utakuwa dhahiri, Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi za Afrika zilizofanikiwa kupeleka kifaa hicho angani, ambazo  ni Algeria, Ethiopia, Kenya, Zimbabwe, Afrika Kusini, Morocco, Misri, Ghana na Nigeria, huku Rwanda ikikusudia kufanya hivyo mwishoni mwa mwaka huu.

Hata hivyo, Rais Samia ameoneka kutofurahia ujenzi wa minara ya mawasiliano unaoendela nchini huku akishauri kuangaliwe namna bora ambayo kwayo nchi inaweza kukusanya mambo yote kwa pamoja bila kuwa na mambo mengi.

“Tatizo nililonalo kichwani kwangu ni moja, nikamuambia Waziri, minara 758 mipya, kuna minara ambayo tayari ipo ndani ya nchi, kuna minara ya Azam Media itakwenda kujengwa na wengine watakuja na minara,” amesema.

Kwa mujibu wa Rais Samia, hali hiyo ya uwepo wa minara mingi ilimfanya kumhoji Waziri mhusika ili kujua kama kunawezakuwa na teknolojia mbadala.

“Nikamuuliza Waziri hakuna teknolojia ya kuchanganya haya yote yakaingia sehemu moja, kwa sababu nchi yote itajaa minara, kila utakapokwenda minara, minara, ukiuliza huu wa wa Azam, Tigo na huu wa Voda, nchi yote itajaa minara,” amehoji Rais Samia.

Amesema ni vyema kama nchi ikatafuta teknolojia itakayoweza kuchanganya vyote kwa pamoja.

“Najua kama Serikali tunajipanga kuja na setelaiti ambayo niwahakikishie kuwa itakuwepo Tanzania, tunajipanga vizuri tumeanza mazungumzo tutajenga setelaiti Tanzania.”

Amesema wakati hilo likifanyika ni vyema kuangalia namna ya kukusanya mambo yote na nchi ikapata huduma zote kwa moja bila ya kuwa na mambo mengi yamesimama.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted