Ukata kusababisha WFP Tanzania kupunguza mgao wa chakula kwa wakimbizi

Zaidi ya wakimbizi 200,000 walioko nchini Tanzania wataanza kupokea nusu mgao wa chakula wanachopatiwa kutokana na ukata unaokabili shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani,...

0

Zaidi ya wakimbizi 200,000 walioko nchini Tanzania wataanza kupokea nusu mgao wa chakula wanachopatiwa kutokana na ukata unaokabili shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP. Asilimia 70 ya wakimbizi hao wanatoka Burundi ilhali asilimia 30 wanatoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Taarifa iliyotolewa jijini Dar es salaam nchini Tanzania na shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP  imesema uamuzi huo unakuja wakati tayari tangu mwaka 2020 walilazimika kupunguza mgao wa chakula.

WFP inasema kwa kawaida kila mkimbizi anatakiwa kupata mlo wa siku wenye kiwango cha chini pendekezwa cha lishe chenye kalori 2,100, lakini kutokana na ukata kuanzia mwezi Machi mwaka huu, mgao ulipunguzwa kutoka kukidhi asilimia 80 ya mahitaji ya kalori hadi asilimia 65.

Kutokana na hali fedha kuwa mbaya, kuanzia mwezi ujao wa Juni mgao  utapunguzwa zaidi hadi asilimia 50 na hivyo wakimbizi kuwa hatarini kukidhi mahitaji  yao ya lishe.

Mkurugenzi Mkazi wa WFP nchini Tanzania Sarah Gordon – Gibson amesema wamepokea kiwango kidogo cha fedha hivyo wanalazimika kuchukua uamuzi mgumu wa kupunguza mgao wakati huu ambapo mahitaji yameongezeka.

Amesema wanahitaji kwa dharura dola milioni 21 kupatia msaada wa chakula zaidi ya wakimbizi 200,000 kwa kipindi cha miezi sita ijayo,  halikadhalika kuepusha njaa kwenye kambi za wakimbizi Tanzania.

Hofu ya Bi. Gordon-Gibson ni kwamba kupunguza mgao kwa kiasi kikubwa kutaweka wakimbizi hatarini hivyo amesihi jamii ya kimataifa, wahisani na sekta binafsi kuchukua hatua haraka za usaidizi ili wakimbizi waweze kukidhi mahitaji yao ya lishe.

Kwa sasa Tanzania inashuhudia ongezeko la wimbi la wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao wanakimbia mapigano jimboni Kivu Kaskazini.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted