LHRC, TAS waitaka Klabu ya Simba kuomba radhi kwa udhalilishaji dhidi ya wenye ualbino.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC), kwa kushirikiana na Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS), kimelaani vikali kitendo kilichotokea Agosti 6, 2023 katika siku ya Simba...

0

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC), kwa kushirikiana na Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS), kimelaani vikali kitendo kilichotokea Agosti 6, 2023 katika siku ya Simba Day, kinachohusisha matumizi ya mtu mwenye ualbino kwa mtindo unaofanana na mtu aliyevaa nepi iliyochafuka jukwaani mbele ya umati wa maelfu ya watu kwenye Uwanja wa Taifa akiwa nusu uchi.

Tukio hili linafuatia tukio lingine lililotokea mwaka jana Agosti 8, 2022, pia siku ya Simba Day, ambapo kulitokea tukio la kutumia jeneza, msalaba na kumdhihaki mtu mwenye ualbino kuwa ni mganga.

Mwenyekiti wa TAS, Godson Mollel amesema viitendo hivyo vinadhalilisha utu wa watu wenye ualbino nchini na kuchangia mijadala mingi ndani ya jamii, yakiwemo majukwaa ya mtandaoni, kuonyesha kejeli kwa watu wenye ualbino, kinyume na misingi ya haki za binadamu.

Mollel amesema kwa miaka mingi kumekuwa na jitihada kubwa za utetezi wa watu wenye ualbino nchini kutokana na historia ya madhila yaliyopelekea watu hao kupoteza maisha,pamoja na idadi kubwa ya wahanga wa vitendo vya ukatili na unyanyapaa.

“Tunasisitiza utani wa jadi uliopo wa Simba na Yanga hauhalalishi vitendo vya kutweza utu wa mtu kwa sababu yoyote ile iwe kwa kukusudia ama kwa kutokukusudia,” amesema Mollel.

Amesema vitendo vya namna hii vinaporuhusiwa kufanywa hususani na taasisi kubwa ya Simba yenye ushawishi kwa jamii inarudisha nyuma kwa kiasi kikubwa jitihada zote zinazofanywa za katika kuhamasisha taswira chanya za watu wenye ualbino.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Anna Henga ametoa rai kwa taasisi zote zenye ushawishi katika jamii hususani timu kubwa za mpira wa miguu kuepukana na vitendo vyenye sura ya udhalilishaji na badala yake wajikite katika kuhamasisha heshima na utu.

Henga amewataka watu wenye ualbino kutochukulia vitendo vya aina hiyo kwa wepesi na badala yake kuvikemea vikali kwa maana na wao ni binadamu kama wengine wenye haki ya kutodharirishwa na kuheshimiwa na utu wao.

Pia amewataka uongozi wa Simba kuomba radhi kwa watu wenye ualbino na umma kwa vitendo vya kutweza utu wao,na kuiomba Serikali pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) kusimamia jambo hilo.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted