Somalia yaamuru kupiga marufuku TikTok, Telegram

Serikali imesema kuwa yalikuwa yanatumiwa na "magaidi" kueneza propaganda

0

Serikali ya Somalia ilitangaza Jumapili kupiga marufuku mitandao ya kijamii ya TikTok na Telegram na programu ya kamari ya mtandaoni, 1XBET, ikisema kuwa yalikuwa yanatumiwa na “magaidi” kueneza propaganda.


Hatua hiyo inakuja kabla ya awamu ya pili ya mashambulizi ya kijeshi yanayotarajiwa dhidi ya Al-Shabaab, kundi la wanamgambo wa Kiislamu ambalo limekuwa likiendesha uasi wa umwagaji damu dhidi ya serikali kuu mjini Mogadishu kwa zaidi ya miaka 15.


Katika taarifa yake, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia iliagiza watoa huduma za intaneti kutekeleza marufuku hiyo ifikapo Agosti 24 la sivyo wachukuliwe hatua za kisheria ambazo hazijatajwa.


Jeshi limekuwa likifanya mashambulizi dhidi ya kundi la Al-Shabaab lenye mafungamano na Al-Qaeda katikati mwa Somalia tangu Agosti mwaka jana, likiungana na wanamgambo wa koo katika operesheni inayoungwa mkono na wanajeshi wa Umoja wa Afrika na mashambulizi ya anga ya Marekani.

Wapiganaji wa Al-Shabaab walifukuzwa kutoka mji mkuu Mogadishu mwaka 2011 lakini bado wanadhibiti maeneo ya mashambani na wanaendelea kufanya mashambulizi mabaya dhidi ya malengo ya kiraia, kisiasa na kijeshi licha ya mashambulizi ya serikali.

Rais Hassan Sheikh Mohamud ameapa kuwaondoa wanajihadi katika nchi hiyo yenye matatizo ya Pembe ya Afrika na anatarajiwa kutangaza hivi karibuni awamu ya pili ya mashambulizi dhidi yao kusini mwa Somalia.


In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted