Uchaguzi mdogo wa Ubunge kufanyika kesho Mbarali

 Kwa mujibu wa taarifa ya NEC iliyotolewa leo ni kwamba uchaguzi wa jimbo hilo la Mbarali unakwenda sambamba na mchakato wa kata sita za Tanzania Bara ambao utahusisha...

0

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema jumla ya wapiga kura 216,282 walioandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wanatarajiwa kupiga kura kesho Jumanne, Septemba 19, 2023 katika uchaguzi mdogo wa marudio wa Mbarali mkoani Mbeya.

 Kwa mujibu wa taarifa ya NEC iliyotolewa leo ni kwamba uchaguzi wa jimbo hilo la Mbarali unakwenda sambamba na mchakato wa kata sita za Tanzania Bara ambao utahusisha vituo 580 vya kupigia kura.

Uchaguzi huo unafanyika ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Francis Mtega aliyefariki dunia Julai Mosi baada ya kugongwa na tekta (Power Tiller) shambani kwake wilayani Mbarali.

Miongoni mwa vyama vinavyoshiriki uchaguzi mdogo wa Mbarali ni pamoja na CCM, ACT- Wazalendo,  Ada – Tadea  ADC, CCK, AAFP,  Demokrasia Makini, DP,  NLD , TLP, UDP, UMD, UPDP na UNDP.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ndio chama pekee ambacho hakikusimamisha mgombea katika nafasi hiyo ambapo uchaguzi unafanyika kesho.

Jaji Mwambegele alivikumbusha vyama vya siasa, wagombea, mawakala wa vyama, wapiga kura na wananchi kwa ujumla kuhakikisha hawapigi kampeni siku ya kupiga kura kwani ni kinyume cha sheria.

“Alama za vyama vya siasa zinazoashiria kampeni kama vile vipeperushi, bendera na mavazi haviruhusiwi kutumika kesho (leo) siku ya uchaguzi,” alisema 

Jaji Mwambegele ameongeza mchakato wa kupiga kura katika maeneo yote ya uchaguzi utafanyika katika vituo vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.

Alifafanua vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa moja kamili asubuhi na kufungwa saa kumi kamili jioni.

“Iwapo, wakati wa kufunga kituo watakuwepo wapiga kura katika mstari ambao wamefika kabla ya saa kumi kamili jioni katika mstari na hawajapiga kura, wataruhusiwa kupiga kura.

“Mtu yeyote hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa wapiga kura baada ya saa kumi kamili jioni,” amesema Jaji Mwambegele.

Jaji Mwambengele amesisitiza watakaoruhusiwa kupiga kura kesho ni wale tu ambao wamo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye kata husika na wana kadi zao za mpiga kura.

“Kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 61(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 pamoja na kifungu cha 62(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292 imeruhusu wapiga kura ambao wamepoteza kadi zao au kadi kuharibika kutumia vitambulisho mbadala.

“Mojawapo ya kitambulisho mbadala ambacho mpiga kura anaweza kutumia ni hati ya kusafiria, keseni ya udereva au Kitambulisho cha Taifa kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida),” alisema.

Jaji Mwambegele amesema ili mtu aruhusiwe kutumia kitambulisho mbadala ni sharti awe ameandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na jina lake lipo katika orodha ya wapiga kura katika kituo anachokwenda kupiga kura.

“Katika kituo cha kupigia kura, kipaumbele kitatolewa kwa wagonjwa, watu wenye ulemavu, wazee, wajawazito na akina mama wanaonyonyesha watakaokwenda na watoto kituoni,” alisema 

Kwa mujibu wa Jaji Mwambegelea kata zitakazofanya uchaguzi ni Nala (Dodoma) Mfaranyaki (Songea) Mwaniko (Mwanza), Old Moshi (Moshi), Marangu Kitowo (Rombo) na  Mtyangimbole (Madaba).

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted