Kibarua kwa bosi mpya wa TANESCO, Rais Samia ampa miezi sita kumaliza tatizo la kukatika umeme Tanzania.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amempa miezi sita Mkurugenzi  mpya wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kukomesha mgao wa umeme unaoendelea kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi...

0

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amempa miezi sita Mkurugenzi  mpya wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kukomesha mgao wa umeme unaoendelea kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi nchini. 

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi wateule aliowateua hivi karibuni huku hoyuba yake ikionekana sana kusisitiza katika Shirika la Umeme nchini.

Amemwambia Boniface Nyamo-Hanga, ambaye ndiye  Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco kuwa kazi yake ya kwanza ni kusimamia ukarabati wa miundombinu ili kukabiliana na tatizo la kukatika kwa umeme linaloendelea hivi sasa.

“Nyamuhanga unakwenda TANESCO nikijua kwamba wewe si mgeni wa TANESCO, unaijua vizuri kwa hiyo utakwenda kuongeza pale Maharage alipofikia.Tuna crisis, crisis ile ni crisis yetu kama taifa si ya mtu, manake mtu mwingine anaeza kusema, Maharage kwa sababu ya kukatikatika kwa umeme ndo maana kaondoshwa, hapana si kwa kozi yake ni kozi yetu kwa pamoja kwamba mitambo ile kwa muda mrefu  haikufanyiwa service” amesema na kuongeza 

“Nakupa miezi sita, nakuangalia pale Tanesco, kazi yako ya kwanza kusimamia ukarabati wa mitambo, baada ya miezi sita nisisikie kelele za kukatika kwa umeme, tutasaidiana nenda najua unaweza,” amesema Rais Samia Ikulu jijini Dar es Salaam.

Ndani ya mwezi mmoja kumekuwa na malalamiko lukuki kutoka kwa watumiaji wa umeme kutokana na mgao wa umeme unaoendelea ambao Maharage alisema unatokana na upungufu wa nishati hiyo kutokana na ukame.

Septemba 23, 2023 Rais Samia alimuondoa Maharage Chande kuwa Mkurugenzi wa Tanesco na kumteua kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kabla ya kumhamisha tena kuwa Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania siku mbili baadaye.

Chande ameondoka Tanesco na Mwenyekiti wa bodi hiyo baada Rais Samia  kumteua Meja Jenerali Paul Simuli kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo akichukua nafasi ya Omar Issa anayeendelea na majukumu mengine ya Ofisi Rais-Tume ya Mipango.

Hali ya upatikanaji umeme kwa sasa nchini si ya kuridhisha kutokana na uwepo wa mgao usio rasmi, wengi hutumia majereta na umeme wa jua kama mbadala wa umeme wa TANESCO kuendesha biashara ama ofisi zao hali iliyozua manung’uniko na lawama kwenda kwenye wizara na shirika lenyewe.

Hata hivyo Rais Samia anapangua hoja hiyo akisema suala la klukatika kwa umeme si la mtu bali linatokana na uchakavu wa mitambo.
“Tatizo la kukatika kwa umeme sio la mtu ni letu .. tumejipanga vizuri tuna mipango ya kuunganisha mikoa kwenye gridi ya taifa ili umeme usikatike,nakupa miezi sita kazi ya kwanza ni ukarabati wa mitambo.” amesema Rais Samia

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted