Matumizi ya kituo cha Kivukoni mwisho leo

Kituo cha daladala cha Kivukoni jijini Dar es Salaam kitafungwa kuanzia kesho Oktoba 21 kupisha upanuzi wa kituo cha mabasi yaendayo haraka cha Kivukoni awamu ya kwanza.

0

Kituo cha daladala cha Kivukoni jijini Dar es Salaam kitafungwa kuanzia kesho Oktoba 21 kupisha upanuzi wa kituo cha mabasi yaendayo haraka cha Kivukoni awamu ya kwanza.

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Mkoa wa Dar es Salaam (DART) umewakumbusha wananchi wakiwamo abiria, wamiliki wa daladala na madereva ambao daladala zao zinafika Kivukoni kuwa mwisho wa matumizi ya kituo hicho ni leo.

Meneja wa Mipango na Usafirishaji Dart, Mohammedi Kuganda amesema tangazo la maelekezo lililotolewa wiki iliyopita halijabadilika na kwamba daladala zilizokuwa zikitumia kituo hicho zimepangiwa vituo vitatu vya dharura. 

Kuganda alisema Dart imeamua kusogeza daladala hizo katika maeneo jirani ya dharura ili kurahisisha hata watu watakaotoka kwenye vivuko kutoka Kigamboni. 

Alitaja vituo vitakavyotumika wakati wa upanuzi wa kituo cha Kivukoni kuwa ni kituo cha muda katika geti la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kitakachotumika kushusha na kupakia abiria wa daladala zitokazo Kigogo Sokoni, Buyuni, Chanika, Machinga Complex, Tabata Chang’ombe na Kinyerezi. 

 “Kituo kingine kitakuwa Mtaa wa Ohio karibu na PPF Tower ambacho kitapokea daladala za Tegeta na Gongo la Mboto na kituo cha mwisho kitakuwa Posta ya zamani karibu na Benki ya NBC kitapokea daladala za Kivule, Kisemvule na Mbande,” alisema Kuganda.

Kwa mujibu wa Dart, lengo la upanuzi huo ni kuweza kupokea mabasi yaendayo haraka kutoka mradi wa awamu ya pili (Mbagala), awamu ya tatu (Gongo la Mboto) na awamu ya nne (Tegeta).

Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Awamu ya Nne unaanzia katika barabara ya Bibi Titi Mohammedi kupitia Maktaba hadi katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi hadi Mwenge mpaka Tegeta na tawi lake la barabara ya Sam Nujoma kutoka Mwenge.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted