Aliyekuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria nchini Tanzania, atuhumiwa kumfanyia ukatili mfanyakazi wake

Gekul ambaye ni Mbunge wa Chama cha Mapinduzi CCM, anatuhumiwa kutoa maelekezo kwa kundi la vijana wake kumwingizia chupa sehemu ya haja kubwa mfanyakazi wake, Hashim Ally au...

0

Jeshi la Polisi Mkoani Manyara limemhoji Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul, kufuatia tuhuma zinazomkabili za ukatili na unyanyasaji dhidi ya mfanyakazi wake, Hashim Ally.

Gekul ambaye ni Mbunge wa Chama cha Mapinduzi CCM, anatuhumiwa kutoa maelekezo kwa kundi la vijana wake kumwingizia chupa sehemu ya haja kubwa mfanyakazi wake, Hashim Ally au kumpiga risasi kwa madai kwamba alitumwa kimkakati kwenda kwenye hoteli yake ya Paleii Lake View Garden.

Hivi sasa kuna  video inasambaa mitandaoni ikimwonyesha Hashim akieleza jinsi alivyofanyiwa ukatili huo na Gekul ambaye hadi Novemba 25, alikuwa ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, kabla ya uteuzi wake kutenguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, usiku wa siku hiyo.

Jana Novemba 26, 2023, Gekul amehojiwa na Jeshi la Polisi mkoani Manyara kufuatia tuhuma hizo zilizoibua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii huku watu wakitoa maoni tofauti.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, George Katabazi amekiri mbunge huyo kufika kituo cha polisi Babati jana majira ya saa 10 jioni kwa ajili ya kutoa maelezo juu ya suala hilo na kisha kuruhusiwa kuondoka.

WANAHARAKATI NA WADAU WA HAKI WATAKA HAKI IPATIKANE

Wakati jeshi la polisi likimhoji Gekul, wanasheria na wanaharakati wa haki za binadamu wametaka hatua zaidi za kisheria zichukuliwe dhidi ya mbunge huyo kama tuhuma zinazomkabili zitathibitika kuwa za kweli.

Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe amesema uamuzi uliotolewa na Rais Samia ambaye ndiyo mamlaka ya uteuzi ulilenga kurejesha imani kwa wananchi kufuatia kile kilichotokea.

“Kwa kuwa mbunge huyo anakabiliwa na tuhuma za uhalifu, uchunguzi ufanyike na hatua zinazofaa zichukuliwe dhidi ya wote waliohusika katika tukio hilo,” amesema.

Massawe amesema ili mradi Waziri anafanya biashara halali na iliyotangazwa na sheria na katiba, hatakiwi kutumia mamlaka yake ya uongozi kuwatia hasara washindani wake.

“Hili limekuwa jambo muda mrefu kwamba viongozi wakuu wa kitaifa wamekuwa wakitumia nyadhifa zao kufaidika na biashara zisizo za haki au kufanya mabadiliko ya kisera na kisheria kwa manufaa yao binafsi,” amesema.

Imeenda mbali zaidi kwa wadau wengine wa haki kupitia mitandao ya kijamii wakikosoa kilichofanywa na mbunge huyo na kudai haki kwa mwathirika.

GEKULU AKANA KUHUSIKA NA TUHUMA

Baada ya taarifa zaidi kusambaa ofisi ya Mbunge huyo kupitia Katibu wake iliandika taarifa ya kukanusha kuhusika kwa mbunge katika kufanya ukatili huo 

Taarifa imedai ofisi ya mbunge imefuatilia kwa kina jambo hilo na kubaini Hashimu Ally alikuwa mtumishi wa Paleii Like View  Garden na alikuwa akijitambulisha kwa jina la Jonathan, baada ya kuacha kazi eneo jingine (jina limehifadhiwa) linalodaiwa kuwa na ushindani wa kibiashara na Paleii Lake View Garden.Inadaiwa maeneo hayo mawili yanafanya kazi inayofanana ya biashara ya chakula.

“Novemba 11, 2023 saa nne asubuhi ndugu aliyejitambulisha Maiko alienda Paleii akiomba kazi kwa madai alipokuwa akifanya kazi awali (inatajwa jina) amefukuzwa. Kijana huyo aliposikilizwa na uongozi wa Paleii, alielezwa hakuna uwezekano wa kupata kazi jambo ambalo hakukubaliana nalo na kutaka kuonana na Pauline Gekul mwenyewe ili aweze kumueleza yaliyomsibu,” imedai sehemu ya taarifa hiyo.

Inadaiwa baada ya kiongozi huyo kurejea akitokea msibani mkoani Arusha, alipata taarifa ya kijana huyo kuomba kazi na kuhusika na vitendo vya kishirikina (kuchota mchanga) ndipo alipompa nafasi ya kumsikiliza.

“Wakati wa maelezo ya kijana huyo, ilibainika alitumwa kimkakati kuchota mchanga yeye na vijana wenzake wawili kwa lengo la kupeleka ukatumike kishirikina,” imedai taarifa hiyo.

Inadaiwa kijana huyo alikiri kuwapo mganga aliyekuwa akisubiri mchanga huo  katika hoteli moja akitokea Iringa.

Taarifa inadai kijana huyo alimtaja mfanyakazi wa Paleii aliyekuwa akifanya naye katika eneo lake la awali anayejitambulisha kwa jina la Jonathan, lakini jina lake halisi ni Hashimu.

Inadaiwa katika taarifa hiyo kwamba mdogo wa mmiliki wa hoteli hiyo anahusika katika kusambaa kwa taarifa zilizozua taharuki juu ya jambo hilo.

Aidha, katibu huyo amedai suala hilo limepelekwa kimrengo wa kisiasa na kuchafua hadhi ya mbunge na taasisi nyingine za chama na Serikali.

“Ndugu wananchi na wakazi wa Babati Mjini kwa kuwa jambo hili lipo kwenye vyombo ya dola, ofisi inawaomba kuendelea kuwa watulivu wakati Jeshi la Polisi linaendelea kushughulikia jambo hili ili kutoa haki kwa pande zote mbili,”

KUHUSU TUHUMA YENYEWE

Kupitia video hiyo Kijana huyo anadai Novemba 11, 2023 aliitwa na mwajiri wake kwenye chumba cha wageni maalumu.

Anadai alimkuta Gekul, katibu wake, mtu mwingine ambaye hakumtaja na kijana mmoja  aliyekuwa amepiga magoti, hivyo naye alitakiwa apige magoti.

Kijana huyo anadai alishutumiwa kwamba aliweka dawa eneo la kazi na kuweka sumu kwenye chakula.

Anadai alikana, ndipo akatajiwa jina la aliyemtuma. Hata hivyo, anadai aliendelea kukana na simu yake ilikaguliwa na hakuna kilichobainika.

Anadai walivuliwa nguo na kuingiziwa chupa, pia walitishiwa kuuawa kwa bastola.

“Aliita polisi wakaja kutuchukua tukakaa polisi siku nne tunahojiwa kuanzia saa mbili mpaka saa nane, siku ya tatu nikaitwa nikaulizwa tena ulitumwa nikakana nikarudishwa polisi,” amedai.

Anadai siku ya nne alitoa mawasiliano ya baba yake kwa ajili ya dhamana, na alipotoka alichukua fomu ya polisi kwa ajili ya matibabu (PF3) kutokana na maumivu aliyopitia.

CCM YAKAA KIKAO

Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara kimefanya kikao chake leo jana  Novemba 26, 2023 kujadili sakata la Mbunge huyo Pauline Gekul anayekabiliwa na tuhuma za ukatili na udhalilishaji, na leo Novemba 27, 2023 kitatoa tamko lake.

Pamoja na kikao hicho kufanyika pia hii leo Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Daniel Chongolo anatarajiwa kuongoza kikao cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kikifuatiwa na vikao vingine viwili kikiwemo kikao cha Kamati Kuu ya CCM kitakachoongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa Samia Suluhu Hassan.

PAULINE GEKULU NI NANI

Pauline Philipo Gekul (amezaliwa Septemba 25, 1978.Ni mwanasiasa nchini Tanzania na mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ambapo kabla ya kuwa MwanaCCM alikuwa kada wa chama Kikuu cha Upinzani chama cha CAHDEMA. 

Amechaguliwa kuwa mbunge wa Babati Mjini kuanzia mwaka 2015 nafasi anayoishikilia hadi sasa. 

Mwaka 2020  alichaguliwa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hayati Dkt John Magufuli kuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi.

Kufuatia kifo cha Rais Magufuli mnamo mwezi Machi 2021, Rais Samia Suluhu baada ya kushika madaraka alimchagua kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Michezo, Sanaa, Utamaduni na Michezo na baadae kumuhamishia katika Wizara ya Katiba na Sheria kama Naibu Waziri nafasi ambayo usiku wa Novemba 25, ilikoma baada ya kufutwa kazi huku sababu zisiwekwe wazi ingawa taarifa zisizo rasmi zinaeleza kufutwa kwake kazi kunafuatia tuhuma za unyanyasaji zinazomkabili.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted