Akamatwa akidaiwa kumbaka mtoto wa miaka saba

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara linamshikilia mtu mmoja (32), akituhumiwa kumbaka mtoto wa miaka saba  ambaye ni mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Nalunga,...

0

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara linamshikilia mtu mmoja (32), akituhumiwa kumbaka mtoto wa miaka saba  ambaye ni mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Nalunga, iliyopo katika Halmashauri ya Mji Nanyamba, mkoani hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 12, 2023,  Kamanda wa Polisi  mkoani hapa, Nicodemus Katembo amesema tukio hilo lilitokea Novemba 18, 2023; saa 7:00 mchana, katika Kijiji cha Nalunga, ambapo inadaiwa kuwa mtuhumiwa ambaye hakutajwa jina, alitenda kosa la kumbaka mtoto huyo na kumsababishia maumivu.

Kwa mujibu wa Kamanda Katembo, mtuhumiwa anadaiwa kutumia mbinu ya kumdanganya mtoto kuwa anaenda kumpa pesa, na ndipo alipopata nafasi ya kutekeleza uharifu huo na kisha kumpa Sh100.

“Siku ya tukio, mtoto huyo alikuwa akicheza na wenzake, ndipo mtuhumiwa akamchukua huku akidanganya kuwa anaenda kumpa hela, alimpeleka porini na kumbaka, kisha akampatia Sh100, huku akimtishia kumuua endapo atasema kwa mtu yeyote,” amesema Kamanda Katembo.

Kwa upande wa mtoto anayedaiwa kufanyiwa ukatili huo (jina limehifadhiwa), amesema: “Alinichukua nikiwa nacheza na wenzangu, akanipeleka kwao kwenye mikorosho, akaniambia niende kuchukua zawadi ya pesa ambayo ni Sh100, alipomaliza aliniambia niondoke na nisiseme kwa mtu, nikisema ataniua na hiyo ilikuwa mara ya pili kunifanyia hukohuko shambani kwao.

Kwa upande wa mama wa mtoto huyo ambaye hakupenda jina lake litajwe,amesema unyama na ukatili aliofanyiwa mtoto wake sio kwamba umembadili mwendo wake pekee, bali hata akili yake haiko sawa.

“Baada ya tukio hata akili zake zimebadilika ukimtuma kikombe anakuletea bakuli yaani hali yake sio nzuri ameathirika kisaikolojia, mpaka urudie sana tena umkalipie ndio anashtuka, lakini hapo mwanzo hakuwa hivyo nimeona mabadiliko baada ya tukio hilo.

“Yaani amezubaa sana hata ukimuita hasikii, labda uitie sana ndio anashtuka kama yuko usingizini, nimejisikia vibaya hata mimi nimeyumba,  mtoto ni mdogo sana kufanyiwa unyama wa namna hiyo, nina hofu ya afya yake, naomba mtoto asaidiewe ili apate ushauri nasaha arudi katika hali yake ya awali,”amesema mama huyo.

 Nae baba wa mtoto huyo, ambaye pia hakutaka kuandikwa jina lake, amesema, “Mwanangu anapenda kucheza sana na wenzake aliporudi hakusema kitu, alipofika nyumbani alikula na kulala, siku iliyofuata aliondoka kwenda kwenye mahafali na huko walimwona akijisaidia haja ndogo huku akilia, watu walipomhoji, ndipo mtoto akasema alichofanyiwa na kutaja eneo ambapo ni kwao na mtuhumiwa.

“Imeniumiza sana, maisha yetu magumu mtoto anafanyiwa kitendo sina uwezo wa kufanya chochote, naomba wadau wa sheria wanisaidie mwanangu ni mdogo amefanyiwa ukatili mkubwa tena katika umri mdogo sana,”amesema baba wa mtoto huyo.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted