Chadema kuhitimisha maandamano ofisi za UN.

Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania, Chama cha Demokrasia na Maendeleo kimesema tayari kimewasilisha barua kwa mamlaka za Polisi nchini humo juu ya kuzijulisha maandalizi yake ya kufanyika...

0

Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania, Chama cha Demokrasia na Maendeleo kimesema tayari kimewasilisha barua kwa mamlaka za Polisi nchini humo juu ya kuzijulisha maandalizi yake ya kufanyika kwa Maandamano ya amani yatakayofanyika January 24 ambapo wameeleza kuwa maandamano hayo yatahitimishwa katika ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika ametoa taarifa hiyo leo ikiwa zimebaki siku saba, kabla ya kufanyika kwa maandamano hayo ya kupinga miswada  mitatu ya sheria za uchaguzi na ugumu wa maisha.

Kwa mujibu wa Mnyika barua hiyo imewasilishwa leo kwa wakuu wa  polisi wa mikoa ya kipolisi ambapo maandaano yatapita.

Januari 13, 2024 Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza vuguvugu la kudai haki litakaloambatana na maandamano ya amani ili kuishinikiza Serikali kuzingatia maoni na mapendekezo ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi kuhusu miswada mitatu.

Miswada hiyo ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani, muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa, yote ya mwaka 2023.

Hii leo CHADEMA imetoa uelekeo wa yatakapoanzia maandamano hayo na kwamba yatakuwa na vituo viwili vikuu yakianzia maeneo ya Mbezi Mwisho na mengine yakianzia Buguruni, yote yatamalizikia ofisi za makao makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini Dar es Salaam.

Mnyika amesema maandamano hayo yatakayoanza saa tatu asubuhi yatakuwa na njia mbili ikiwemo ya Mbezi yakipitia Barabara ya Morogoro, Shekilango, Igesa- Sinza na kuishia Barabara ya Sam Nujoma ambako ujumbe wa maandamano utakapokelewa kwenye ofisi za UN.

“Tumeshapeleka barua kwa Jeshi la polisi kwa mujibu wa kifungu cha 11 (4) cha Sheria ya Vyama vya Siasa toleo la mwaka 2019 kuhusu kufanyika kwa maandamano haya, tumezitaarifu mamlaka mbalimbali za polisi kuhusu njia zitakazotumika katika maandamano ya amani.

“Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, taarifa za maandamano zinatolewa kwa wakuu wa polisi wa wilaya (OCD), tumeandika barua kwenda kwa OCD wa Gogoni, Buguruni, Oysterbay, Mburahati, Msimbazi, kisha nakala tumezipeleka kwa makamanda wa polisi wa mikoa ya kipolisi Ilala na Kinondoni,” amesema Mnyika.

Hata hivyo, wakati Chadema ikiendelea na mipango hiyo, Serikali imesema hakuna haja ya kuondoa miswada hiyo bungeni badala yake utoaji wa maoni unaendelea kwa mujibu wa taratibu.

Itakumbukwa kuwa wakati CHADEMA imetangaza kufanya maandamano tayari Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, imeonekana kuweka vizuizi vinavyoashiria kukwamisha maandamano hayo kwa kuutangazia umma kwamba kutakua na zoezi la usafi litakalofanywa na Vyombo vya Ulinzi nchini jambo ambalo limetajwa ni kinyume na Sheria.

Macho na Masikio ya wengi kwa sasa ni kuelekea maandamano hayo huku wengi wakiwa na shauku ya kutaka kujua je ni kweli yatafanyika? Na hii ni kutokana na kwamba si mara ya kwanza kwa CHADEMA kutangaza maandamano, moja ya maandamano yaliyochochewa na hatimaye hayakufanyika ni yale ya UKUTA.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted