Mzee Mwinyi afariki dunia kwa saratani ya mapafu

Ali Hassan Mwinyi maarufu Mzee Rukhsa alikuwa rais wa awamu ya pili ncini Tanzania aliyehudumu madarakani kwa miaka 10 kutoka mwaka 1985 mpaka 1995.

0

“Leo nina miaka karibu 94, sina siku nyingi za kuiacha dunia. Sitaki niende huko napoenda na aibu nyuma yangu.

“Maisha ya mwanadamu ni hadithi tu hapa ulimwenguni, basi ewe ndugu yangu kuwa hadithi nzuri kwa hao watakaosimuliwa…” hii ni moja ya nukuu maarufu zaidi ya hayati Ali Hassan Mwinyi katika miaka ya hivi karibuni.

Ama kweli maisha ya mwanadamu ni hadithi tu hapa ulimwenguni, hadithi ya maisha ya Mzee Mwinyi ilihitimishwa jana Februari 29, saa 11:30 jioni baada ya mauti kumfika kiongozi huyo mashughuli nchini Tanzania.

Ali Hassan Mwinyi maarufu Mzee Rukhsa alikuwa rais wa awamu ya pili ncini Tanzania aliyehudumu madarakani kwa miaka 10 kutoka mwaka 1985 mpaka 1995.

Hadithi ya maisha yake ilianza kuandikwa Mei 8 mwaka 1925, alipozaliwa katika kijiji cha Kivule katika eneo la kisiju Pwani, Wilaya ya Mkuranga katika Pwani ya Tanzania.

Wengi wanamfahamu kwa jina la Ali Hassan Mwinyi ambalo ndilo maarufu, lakini wengine wanamfahamu kama mzee wa Ruksa, lakini Hayati mwinyi enzi za utoto wake alipewa majina mengi na moja ya majina hayo ambayo  alipewa na wazazi wake ni jina la Sihaba, likiwa na maana ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kuwajaalia mtoto wa kiume, wazazi wake mpaka anazaliwa yeye walikuwa na watoto wa kike tu hivyo ujio wake duniani ulikuwa na neema kwa wazazi wake na ndugu zake waliomtangulia.

Alipotimu miaka 4 safari ya maisha ya Mzee Mwinyi iliingia katika hatua muhimu ambayo ilibadili mustakabali mzima wa maisha yake yote ya baadaye. Baba yake, Mzee Hassan Mwinyi aliamua kumpeleka kijana huyo visiwani Zanzibar ili akapate malezi na mafunzo ya kidini kwani baba yake alitamani awe mchamungu na mwanazuoni mkubwa.

Na ili kufikia azma hiyo, Baba yake alitamani asome dini mpaka kufikia katika chuo maarufu cha enzi hizo visiwani Zanzibar cha Ukutani.

“Kuhusu elimu ya dini, zama zile wasomi wakubwa walipatikana miongoni mwa watu waliosoma Chuo cha Ukutani, Unguja. Enzi zile, kwa watu wa Zanzibar na Afrika ya Mashariki, umashuhuri wa chuo hicho kwa elimu ya dini ulifanana na ule wa Vyuo Vikuu vya Oxford na Cambridge vya Uingereza kwa elimu ya dunia.

Ndio maana nilipotimia umri wa miaka minne baba alinifungia safari ya Unguja ili nikaanze kusoma katika vyuo vya chini kwanza ili mwishowe nami nifike Ukutani,” ameandika Mzee Mwinyi katika kitabu chake.

Baada ya kusoma kwa miaka minne katika shule hiyo Mzee Mwinyi alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi wawili tu waliochaguliwa kuendelea na masomo katika Shule ya Kati ya Dole ambayo ilikuwa ni ya bweni na kusoma hapo mpaka darasa la nane.

Mzee Mwinyi anaeleza katika kitabu cha maisha yake kuwa mpaka anamaliza masomo yake ya elimu ya msingi alikuwa hakosi katika orodha ya wanafunzi watatu bora.

Baada ya kumaliza masomo ya msingi aliendelea na masomo ya sekondari na baaadaye mafunzo ya awali ya ualimu hapo hapo Dole mwaka 1944.

Mzee Mwinyi alianza rasmi kazi ya ualimu mara tu baada ya kuhitimu masomo. Baada ya kufanya kazi kwa miaka 10 Mzee Mwinyi alipelekwa masomoni nchini Uingereza katika Chuo Kikuu cha Durham kuendelea na masomo ya ualimu kati ya mwaka 1954 na 1956.

Kati ya mwaka wa 1961 na 1962 Mzee Mwinyi alirejea nchini Uingereza kwa mafunzo zaidi katika Chuo Kikuu cha Hull, na aliporejea Zanzibar aliteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo cha Ualimu , kazi aliyoifanya mpaka mwaka 1964 yalipotokea Mapinduzi ya Zanzibar.

Mzee Mwinyi aliupenda ualimu na alikipenda Kiswahili, haikuwa ajabu mara kwa mara kumsikia katika uhai wake akikemea matumiza mabovu ya lugha.

Hivyo kwa maana nyingine unaweza kumuita Mzee Mwinyi mwalimu Mwinyi taaluma ambayo aliijenga moyoni mwake tangu anasoma.

Safari ya Maisha ya kisiasa ya Mzee Mwinyi

 Januari 12, 1964 visiwani Zanzibar kulitokea mapinduzi  ambapo utawala wa Kisultani uliangushwa, watumishi wengi wa umma hasa raia wa Uingereza waliondoka visiwani humo na kuacha ombwe la uongozi serikalini.

Kufuatia hali hiyo visiwa vya Zanzibar vikawa na kazi ya kujijenga kwa utawala wake kwa kuanza kuongeza watumishi serikalini ili kuisaidia nchi. Mzee Mwinyi alikuwa mmoja wao ambye aliteuliwa na aliyekuwa rais wa kwanza wa Zanzibar Abedi Amani Karume kuwa Katibu Mkuu katika Wizara ya Elimu.

Mwezi Aprili 1964, serikali za Zanzibar chini ya hayati Karume na ya Tanganyika chini ya Mwalimu Julius Nyerere zikaungana kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Miaka sita baadaye, Disemba 1970 akateuliwa kuwa Waziri katika serikali ya muungano na kuhudumu katika wizara mbali mbali, akianzia katika Ofisi ya Rais, kisha Afya kutoka 1972 mpaka 1975.

Mwaka 1975 Mwalimu Nyerere alimteua Mzee Mwinyi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi nafasi ambayo alijiuzulu mwaka 1977  kufuatia ukiukwaji wa haki za binadamu wa vyombo vya dola katika operesheni maalumu ya kudhibiti mauaji ya watu wakongwe katika mikoa ya kanda ya ziwa nchini Tanzania.

Baada ya kujiuzulu, Mwinyi aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri kutoka mwaka 1978 mpaka 1981.

Hata hivyo mwaka 1984 Mwinyi alirejea katika Baraza la Mawaziri la Nyerere mara tu aliporejea kutoka Misri 

Mwaka 1985, ulikuwa mwaka muhimu katika historia ya siasa za Tanzania, Mwalimu Nyerere alikuwa anang’atuka madarakani.

Katika kitabu chake Mzee Mwinyi anaeleza kuwa wengi, akiwemo yeye mwenyewe, waliamini aliyekuwa Waziri Mkuu wa wakati huo na mwanadiplomasia mbobevu Dkt Salim Ahmed Salim alikuwa anaenda kumrithi Mwalimu.

Mambo hayakuwa kama walivyofikiria  kwa mujibu wa Mzee Mwinyi baadhi ya Wazee wenye msimamo mkali wa kihafidhina ndani ya CCM walimkataa Dkt Salim na Mwalimu Nyerere alilazimika kukubali ili kulinda umoja wa chama hicho. Bahati kwa mara nyingine tena ikamwangukia Mzee Mwinyi.

Ndipo hapo sasa alipokea kijiti cha Urais kutoka kwa Mwalimu Nyerere, wakati ambapo ulikuwa mgumu sana kwake kutokana na kwamba Mzee Mwinyi aliingia madarakani wakati ambapo Tanzania ilikuwa ikipitia wakati mgumu kiuchumi. 

Alilazimika kufanya mabadiliko ya kisera na kisiasa ili kuchochea ukuaji wa uchumi.

Mabadiliko hayo hayakuwa rahisi kutokea kwa kuwa bado ndani ya serikali na chama cha CCM kulikuwepo na wale walioamini na kutaka kuendelea kwa mfumo wa Ujamaa.

Hata hivyo, Mzee Mwinyi alishikilia hatamu za uongozi barabara na kutekeleza alichokiamini, hali iliyofanya utawala wake ujitanabaishe zaidi na mabadiliko kuanzia ya kisera, kisiasa na kiuchumi.

Ni wakati wa utawala wake ndipo serikali ilipoanza kuchukua hatua za kurudi nyuma katika kuendesha uchumi moja kwa moja na kuruhusu sekta binafsi kuingia, mfumo wa vyama vingi kurejea pamoja na kuruhusiwa kwa vyombo vya habari binafsi.

Hayo na mengineyo yakampatia jina ambalo litaendelea kuwa kielelezo cha uongozi wake: Mzee Rukhsa.

Katika kitabu chake, anataja mambo kadhaa kuwa ni changamoto alizokutana nazo akiwa uongozini, baadhi ni mpasuko katika muungano (wa Zanzibar na Tanzania bara), migogoro ya udini, madawa ya kulevya, ugonjwa wa Ukimwi na migomo ya wanafunzi na wafanyakazi.

Ali Hassan Mwinyi alifariki dunia jana akiwa na miaka 98, katika hospitali ya Mzena jijini Dar es salaam, ambako alilazwa kwa matibabu ya kansa ya mapafu.

Mwili wake unaagwa leo jijini Dar es salaa katika uwanja wa Uhuru mara baada ya sala ya Ijumaa ambapo utaswaliwa katika msikiti wa BAKWATA Kinondoni.

Mara baada ya wakazi wa Dar es salaam kupata nafasi ya kuaga mwili wa Hayati Mzee Mwinyi utapelekwa Zanzibar na kuzikwa kesho Machi 2,2024 huko Unguja.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted