ACT Wazalendo waitaka Serikali itekeleze ahadi yake ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa

Chama cha ACT Wazalendo  kimeitaka Serikali kutekeleza ahadi yake ya kutunga sheria ya kuiwezesha Tume Huru ya Uchaguzi kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

0

Chama cha ACT Wazalendo  kimeitaka Serikali kutekeleza ahadi yake ya kutunga sheria ya kuiwezesha Tume Huru ya Uchaguzi kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu Mwenyekiti Bara wa chama hicho, Isihaka Mchinjita kwenye mapokezi ya kumpongeza kwa kuchaguliwa na Mkutano Mkuu Taifa yaliyofanyika katika ofisi ya Mkoa wa Lindi iliyopo Lindi Mjini jana Machi 17.

“Tarehe 2 Februari 2024 kwenye mchakato wa kutunga Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi Serikali ilileta jedwali la maboresho ili kuipa dhamana Tume ya Taifa ya Uchaguzi kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa serikali za vijiji, mitaa na vitongoji kwa kuzingatia utaratibu utakaoainishwa na Sheria itakayotungwa na Bunge,” alisema Mchinjita

“Kwa bahati mbaya, miswada ya Tume ya Uchaguzi na Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani bado haijasainiwa na Rais kuwa sheria hadi sasa. Hatujui ni maboresho gani hasa yamepitishwa kuwa sheria. pili, hadi sasa, serikali haijaanza mchakato wa sheria iliyoahidiwa bungeni ya kuipa madaraka Tume ya Uchaguzi kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Tunaona dalili za serikali kupata kigugumizi katika kutekeleza ahadi yake”

“Ni muhimu Bunge lisimame kidete kuhakikisha maboresho yaliyofanyika Bungeni ya kuipa dhamana Tume ya Taifa ya Uchaguzi kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa yanazingatiwa. Ni muhimu mchakato wa kutunga sheria kwa suala hilo uanze sasa. ACT Wazalendo tumeshaiagiza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Chama kuainisha vipaumbele vya ACT Wazalendo tunavyotaka kuwepo kwenye Sheria hiyo” alisisitiza Ndugu Isihaka Mchinjita.

Katika hatua nyingine, Ndugu Mchinjita amesema kuwa kwa kushirikiana na viongozi wenzake na Baraza Kivuli la Mawaziri la ACT Wazalendo, atahakikisha kuwa ACT Wazalendo kinaendelea kuwa chama kinara katika kuzisemea kero za wananchi wa Tanzania.
“Mfano hapa Lindi, mradi wa kuchakata gesi wa LNG ulishafikia hatua ya Serikali kusaini HGA wakati waziri akiwa ndugu January Makamba. Amekuja waziri mpya amerudisha nyuma mjadala kana kwamba tumekuwa na wataalam wapya wanaomshauri 3aziri. Wazalendo tunaitaka Serikali iharakishe mazungumzo ili mradi uanze kwa maendeleo ya nchi yetu, Lindi na kusini kwa ujumla,” alisisitiza Mchinjita.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted