Lissu, Mbowe kuongoza maandamano ingwe ya tatu katika mikoa 13 ya Tanzania bara

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es salaam katika makao makuu ya chama hicho Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje bwana John Mrema amesema hatua hiyo...

0

Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania chama cha CHADEMA, kimetangaza ratiba ya ingwe nyingine ya maandamano yatakayoanza kufanyika Aprili 22,2024 hadi Aprili 30 kwa awamu ya kwanza  katika mikoa ya Tanzania.

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es salaam katika makao makuu ya chama hicho Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje bwana John Mrema amesema hatua hiyo ni mwendelezo wa ajenda zao na makubaliano yaliyofanyika katika kikao kilichofanyika mkoani Mtwara maarufu Azimio la Mtwara na kwamba kamwe hawatarudi nyuma.

Kwa mujibu wa Mrema maandamano hayo wameyagawa katika awamu mbili ambapo wamu ya kwanza itahusisha kanda nne ambazo ni Kanda ya Serengeti yenye mikoa ya Shinyanga, Musoma na Simiyu, Kanda ya Victoria yenye mikoa ya Kagera, Geita na Mwanza,Kanda ya Kati yenye mikoa ya Singida, Dodoma na Morogoro na Kanda ya Kaskazini yenye mikoa ya  Arusha, Manyara, Tanga na Kilimanjaro na kanda zote zitaongozwa na viongozi wakuu wa CHADEMA ambao ni Mwenyekiti Freeman Mbowe na Makamu Mwenyekiti Tundu Lissu.

Mrema amesema katika mgawanyo huo Aprili 22, Freeman Mbowe ataongoza maandamano mkoa wa Kagera, Aprili 23 ataongoza maandamano mkoa wa Shinyanga, Aprili 24 ataongoza maandamano Geita Mjini, Aprili 25 ataongoza maandamano Bariadi Mjini, Aprili 26, ataongoza maandamano Musoma Mjini, Aprili 27 ataongoza maandamano Mwanza katika wilaya ya Sengerema, Aprili 29 ataongoza maandamano mkoani Tanga na Aprili 30 atahitimisha maandamando mkoa wa Kilimanjaro.

Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu, Aprili 25 ataongoza maandamano mkoa wa Arusha, Aprili 26 ataongoza maandamano mkoa wa Manyara, Aprili 27 ataongoza maandamano mkoa wa Singida mjini, Aprili 29 ataongoza maandamano mkoa wa Dodoma na atahitimisha maandamano hayo Aprili 30 mkoani Morogoro.  

Lengo la kugawa maandamano hayo na kila kanda kuongozwa na viongozi wakuu ni kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo hali ya hewa na mvua zinazoendelea kunyesha nchini kote.

Chadema imedai kuwa bado Serikali haijachukua hatua zozote hadi sasa licha ya kuwasilisha madai yao kupitia maandamano ya awamu ya kwanza 

Itakumbukwa kuwa ajenda za maandamano hayo ni kupinga ugumu wa maisha, kupinga sheria inayotumika sasa ya Kikokotoo, madai ya Katiba mpya lakini pia matumizi ya anasa ya rasilimali za umma.

Kwa mara ya kwanza CHADEMA ilifanya maandamano Januari 24 jijini Dar es salaam na baadae kuelekea katika mikoa ya Arusha, Mwanza na Mbeya ambako kote huko waandamanaji waliandamana kwa mabango yenye jumbe tofauti ya kuishinikiza Serikali iliyopo madarakani.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted