, , ,

LHRC yataja dosari 12 za kisheria katika hukumu ya Lissu, yataka mapitio

Asia Gamba Avatar

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeibua hoja 12 za kisheria kuhusu mwenendo wa kesi ya uhaini iliyokuwa ikimkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antipas Lissu, kikisema baadhi ya hatua zilizochukuliwa wakati wa kesi hiyo ziliibua maswali kuhusu uzingatiaji wa haki za mshtakiwa na misingi ya utoaji wa haki nchini Tanzania.

Katika taarifa yake iliyotolewa jijini Dar es Salaam leo Alhamisi, Novemba 12, 2026, LHRC imesema ilifuatilia mwenendo wa kesi hiyo kuanzia Aprili 9, 2025, siku ambayo Lissu alikamatwa akiwa katika ziara ya chama chake wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma, hadi Novemba 6, 2026, mahakama ilipotoa hukumu na kumhukumu kifungo cha miaka minne jela.

Kwa mujibu wa LHRC kupitia Mkurugenzi wake Anna Henga, Lissu alikuwa ametumia takribani siku 577 mahabusu kabla ya hukumu hiyo kutolewa, kipindi ambacho kituo hicho kinasema kilikuwa kirefu na kilimtenganisha na familia yake pamoja na maisha yake ya kawaida.

Katika tathmini yake, LHRC imesema mojawapo ya hoja ilizobaini ni namna Lissu alivyokamatwa, ikidai kuwa maafisa wa polisi hawakumweleza sababu za kukamatwa kwake, kinyume na kifungu cha 241 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai pamoja na Kanuni za Kudumu za Jeshi la Polisi.

Kituo hicho pia kimehoji matumizi ya mabomu ya machozi yaliyofanywa na polisi wakati wa mkutano wa hadhara aliokuwa akihutubia Lissu Mbinga, kikisema hatua hiyo ilisababisha baadhi ya wananchi kujeruhiwa na wengine kukamatwa. LHRC imesema tukio hilo lilizua maswali kuhusu ulazima na uwiano wa nguvu zilizotumika katika operesheni hiyo.

Hoja nyingine iliyotajwa ni muda wa kukamilisha upelelezi. LHRC imesema mwongozo wa Mkurugenzi wa Mashtaka wa mwaka 2022 unaelekeza upelelezi wa kesi zinazofunguliwa kabla haujakamilika kukamilishwa ndani ya siku zisizozidi 90.

Hata hivyo, kituo hicho kimesema mwenendo wa awali wa shauri la Lissu ulichukua takribani miezi mitano bila upelelezi kukamilika, huku upande wa mashtaka ukiwa haujaomba muda wa nyongeza kama mwongozo unavyoruhusu.
LHRC pia imesema haki ya Lissu kujitetea iliathiriwa baada ya mahakama kukataa kurekodi majina ya baadhi ya mashahidi aliowataja katika hatua ya awali ya shauri. Kwa mujibu wa kituo hicho, Lissu alipowataja tena mashahidi hao katika Mahakama Kuu, upande wa mashtaka ulipinga hoja hiyo kwa maelezo kuwa hawakuwa wametajwa wakati wa mwenendo wa awali.

Katika hatua nyingine, LHRC imeibua maswali kuhusu jaribio la kuendesha kwa njia ya mtandao shauri jingine la uchochezi lililokuwa likimkabili Lissu katika Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam. Kituo hicho kimesema hatua hiyo ilizua wasiwasi kuhusu uwazi wa mwenendo wa mashauri na uwezo wa mshtakiwa kushiriki kikamilifu katika kesi yake. Hata hivyo, baada ya kupingwa, usikilizwaji ulirejeshwa katika utaratibu wa kawaida.

Kituo hicho pia kimeeleza wasiwasi kuhusu kukamatwa na kurejeshwa nchini kwa baadhi ya watu waliotaka kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo, wakiwamo wakili na mwanasiasa wa Kenya Martha Karua, aliyekuwa Jaji Mkuu wa Kenya Willy Mutunga, mwanaharakati Boniface Mwangi na mwandishi wa habari wa Uganda Agather Atuhaire.

LHRC imesema matukio hayo, pamoja na madai ya kutekwa na kuteswa kwa baadhi ya watu hao kabla ya kuonekana katika mpaka wa Tanzania na Uganda, yaliibua maswali kuhusu usalama wa waangalizi wa kimataifa na mazingira ya kufuatilia mwenendo wa mashauri ya mahakama nchini.

Katika masuala yanayohusu mazingira ya Lissu akiwa gerezani, LHRC imesema ilibaini madai ya kuhamishwa kutoka Gereza la Keko kwenda Ukonga bila taarifa kwa mawakili na familia yake, pamoja na changamoto za mawasiliano ya siri kati yake na mawakili wake.

Kituo hicho kimesema suala la kuingiliwa kwa mawasiliano ya siri kati ya mteja na wakili, pamoja na baadhi ya mawakili kunyimwa fursa ya kumwona Lissu, lilijadiliwa katika Shauri la Kikatiba Na. 7300/2026, ambalo Mahakama Kuu iliamua kuwa hatua hizo zilikiuka haki zake.

Hoja nyingine ni madai ya Lissu kuwekwa katika mazingira ya gereza pamoja na wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kifo wakati yeye alikuwa bado mshtakiwa. LHRC imesema hatua hiyo ilizua maswali kuhusu uzingatiaji wa Sheria ya Magereza na kanuni ya kutambua kuwa mtu hana hatia hadi ithibitishwe vinginevyo.

Kituo hicho pia kimehoji matumizi ya mashahidi wa kificho katika kesi hiyo, kikisema mashahidi wa upande wa mashtaka walitoa ushahidi wakiwa wamefichwa nyuma ya kizimba maalumu, hali ambayo kwa mtazamo wake ilipunguza uwezo wa Lissu kuwatambua, kutathmini uaminifu wao na kuwauliza maswali kwa ufanisi.

Aidha, LHRC imesema jaribio la upande wa mashtaka kuwasilisha ushahidi kuhusu matukio ya Oktoba 29, 2025, takribani miezi sita baada ya Lissu kukamatwa, lilizua hoja kuhusu uhalali wa ushahidi huo. Mahakama Kuu ilikataa jaribio hilo, lakini maombi ya mapitio yaliyowasilishwa na upande wa mashtaka katika Mahakama ya Rufani yalisababisha mwenendo wa kesi kusimama kwa takribani miezi sita.

LHRC imetaja pia madai ya kuzuiwa kwa viongozi wa dini kumtembelea Lissu gerezani, ikiwamo tukio la Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Singida kuzuiwa kuingia Gereza la Ukonga alipokwenda kumtembelea. Kituo hicho kimesema hali hiyo ilizua maswali kuhusu haki ya uhuru wa kuabudu inayolindwa na Ibara ya 19 ya Katiba.

-LHRC yahoji matumizi ya kosa dogo katika hukumu ya Novemba 6-

Mbali na tathmini ya mwenendo wa kesi, LHRC imeeleza kuwa ina maswali kuhusu namna Mahakama Kuu ilivyofikia uamuzi wa kumtia hatiani Lissu kwa kosa dogo baada ya kumwachia huru katika shtaka la uhaini.

Mahakama ilisema upande wa Jamhuri ulishindwa kuthibitisha shtaka la uhaini pasipo kuacha shaka yoyote. Hata hivyo, ilitumia kifungu cha 319 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na kumtia hatiani Lissu kwa kosa dogo la uchochezi, kisha kumhukumu kifungo cha miaka minne.

LHRC imesema matumizi ya dhana hiyo yanapaswa kuzingatia masharti kadhaa, yakiwamo kuwepo kwa ushahidi unaothibitisha kosa dogo, uhusiano wa kisheria kati ya kosa kubwa na kosa dogo, pamoja na mshtakiwa kupewa taarifa na nafasi ya kutosha kujiandaa kujibu shtaka hilo.
Kituo hicho kimesema katika ukurasa wa 122 wa hukumu, Lissu alipinga kuwepo na matumizi ya dhana ya kosa dogo, huku upande wa Jamhuri ukiwa haukutoa hoja kuhusu suala hilo. Kwa mtazamo wa LHRC, mazingira hayo yanazua maswali kuhusu kama Lissu alipewa nafasi ya kutosha kujitetea dhidi ya kosa ambalo hatimaye alikutwa nalo na hatia.

Katika suala la adhabu, LHRC imesema Lissu alikuwa mkosaji wa mara ya kwanza na kwamba mahakama haikuzingatia ipasavyo mwongozo wa Mahakama ya Rufani wa Mei 22, 2020, unaoelekeza kuwa faini inapaswa kupewa kipaumbele kwa wakosaji wa mara ya kwanza pale sheria inapotoa nafasi ya kuchagua kati ya faini, kifungo au vyote viwili.

Kituo hicho pia kimesema mahakama haikuzingatia kikamilifu siku takribani 577 ambazo Lissu alizitumia mahabusu kabla ya hukumu. LHRC imetaja uamuzi wa shauri la Nyanzala Madaha dhidi ya Jamhuri, Rufaa ya Jinai Na. 65 ya mwaka 2005, pamoja na Mwongozo wa Utoaji Adhabu wa Mahakama Kuu wa mwaka 2023, kama sehemu ya misingi inayopaswa kuzingatiwa katika suala hilo.

-Wito kwa DPP kupitia upya mashtaka ya Uhaini na Ugaidi-

Kutokana na hoja hizo, LHRC imetoa mapendekezo kadhaa, ikiwamo kumtaka Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kupitia upya mashauri yote ya uhaini yaliyofunguliwa chini ya kifungu cha 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu, kwa kuzingatia tafsiri ya Mahakama Kuu kuhusu vigezo vinavyopaswa kuthibitishwa ili mtu apatikane na hatia ya kosa hilo.

Pia imeitaka Ofisi ya Jaji Mkuu kutoa mwongozo kuhusu matumizi ya kifungu cha 319 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, hasa masharti yanayopaswa kuzingatiwa na mahakama kabla ya kumtia hatiani mshtakiwa kwa kosa dogo badala ya kosa kubwa aliloshtakiwa nalo.

LHRC imeitaka pia DPP kupitia upya mashauri ya ugaidi ambayo bado hayajaanza kusikilizwa, hususan yale ambayo muda wa upelelezi uliowekwa katika miongozo ya kisheria umepita. Imependekeza mashauri yenye ushahidi wa kutosha yaendelee kwa mujibu wa sheria, huku yale yasiyo na ushahidi yakiondolewa.

Mapendekezo mengine yanahusu vyombo vya dola kutofautisha kati ya maoni ya kisiasa na makosa ya jinai, polisi kuzingatia sheria wakati wa ukamataji na matumizi ya nguvu, pamoja na mamlaka za magereza kuheshimu haki za wafungwa na mahabusu, ikiwamo kupata huduma za kisheria, kuwasiliana na familia na kupata huduma za kiroho.

Our Correspondent Avatar