Rais wa zamani wa DR Congo afunguliwa mashtaka ICC

Rais wa zamani wa DR Congo afunguliwa mashtaka ICC

0
Joseph Kabila, Rais wa zamani DR Congo

Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Joseph Kabila huenda akajipata taabani baada ya waathiriwa wa maovu wanayodai alitenda kuwasilisha kesi dhidi yake, katika Mahakama ya Makosa ya Jinai (ICC) wakimshtaki kwa kuua na kutesa jamaa zao.

Malalamiko hayo yaliwasilishwa Septemba 16. Kati ya wale ambao wamejumuishwa kwenye mashtaka hayo ni viongozi wakuu waliokuwa katika serikali ya Kabila ikiwemo Emmanuel Ramazani Shadary, aliyeungwa mkono na Kabila katika kuwania kiti cha urais mwaka 2019 ila akashindwa katika kinyang’anyiro hicho na rais wa sasa Felix Tshisekedi. Bwana Shadary alikuwa Waziri wa Usalama wa Ndani kabla kuwania kiti cha urais.

Wanaolalamika ni jamaa za waathiriwa wa mapigano ya 2016-2017 kati ya raia, polisi na maafisa wa jeshi katika mkoa wa Kasai.

Waathiriwa hao wametoa wito kwa mwendesha mashtaka wa ICC kufanya uchunguzi ili kuwahukumu watuhumiwa na washtakiwa, lakini pia kutambua haki ya waathiriwa kwa ajili ya kupata fidia.Waathiriwa hao wanasema, Kasai ilikuwa eneo la uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa miaka miwili.

Waathiriwa wanadai kuwa Kabila, hakufanya uchunguzi wowote dhidi ya unyama uliotendeka licha ya wito uliotolewa kwa viongozi wa kisiasa na mahakama kufanya hivyo.

Kundi hilo liliwasilisha malalamiko yao mara ya kwanza mwaka wa 2019 dhidi ya jeshi la Congo kupitia mkaguzi wa juu wa jeshi kutoka Kasai ila hawakufaulu.

“Chama chetu kiliamua na kuwasilisha malalamiko haya dhidi ya Joseph Kabila kwa ofisi ya mwendesha mashtaka wa ICC mjini Hague kwa niaba ya waathiriwa 20,000 wa mateso hayo,” amesema Mhyrhand Mulumba, mkuu wa chama hicho.

Kati ya wale walioshtakiwa ni Kalev Mutond, mkuu wa huduma za ujasusi katika utawala wa Kabila, ambaye kwa sasa yupo mafichoni.

Wandani wa Kabila, wamepinga hatua hiyo ya kuwasilishwa kwa malalamiko dhidi yao kwa mahakama ya ICC.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted