Mwongozo wa misamaha ya kodi mbioni kukamilika

MWONGOZO WA MISAMAHA YA KODI MBIONI KUKAMILIKA

0
Rais Samia Suluhu Hassan

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha mwongozo wa misamaha ya kodi kwa mashirika yasiyo ya kiserikali huku akiyataka mashirika hayo kupunguza utegemezi wa fedha kutoka kwa wahisani.

Rais Samia ameyasema hayo leo alipokuwa kwenye mkutano mkuu wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (Nacongo) uliozikutanisha NGO zote zinazofanya kazi hapa nchini, ambapo amesema zipo changamoto kwenye mifumo ya kodi kwa baadhi ya taasisi zinazostahili kupata msamaha wa kodi na tayari Serikali imeanza kufanyia kazi masuala yote hayo.

“Kuhusu msamaha wa kodi kwa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ambayo yanafanya kazi kwa hisani tayari tumeshakamilisha kuandaa kitini kinachotoa mwongozo wa namna mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yatanufaika na misamaha ya kodi,” amesema Rais Samia.


“Tuko katika hatua za mwisho za kumalizia,” amesema kiongozi huyo mkuu wa nchi leo Septemba 30, 2021 aliposhiriki mkutano wa mwaka wa jukwaa la mashirika yasiyo ya kiserikali jijini Dodoma.

Rais Samia amesema huenda mwongozo huo utapunguza malalamiko ya baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali kudaiwa kutozwa kodi wakati hayaingizi faida na yanategemea misaada ya washirika wa maendeleo.
Aidha, Rais ameyataka mashirika hayo kupunguza utegemezi na kubaki katika malengo ya kuanzishwa kwao ili kutimiza kwa ukamilifu ajenda za maendeleo.

“Nayahimiza mashirika yasiyo ya Serikali hususan ya ndani, kupunguza utegemezi. Ajenda za kidunia zinavyobadilika, wahisani wanabadilisha sera zao za kutoa fedha, unajikuta lile uliloanzishia taasisi, si kipaumbele kwao, mnajikuta hamna fedha za kujiendesha,” amesema Rais.


Takwimu zinaonyesha Tanzania bara ina mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyosajiliwa yapatayo 11,603 na yametoa ajira za moja kwa moja 17,836.


Pamoja na hayo Rais Samia ameziagiza sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa mashirika hayo katika kutoa kwa wakati vibali vya utekelezaji wa miradi wanayoibuni ili kujenga Taifa kwa pamoja.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted