Mahakama yasomewa kielelezo cha kwanza cha ushahidi

Mahakama Kuu, Divisheni ya makosa Rushwa na Uhujumu Uchumi imesomewa kielelezo cha kwanza cha ushahidi wa Jamhuri katika kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya ugaidi, inayomkabili kiongozi...

0

Mahakama Kuu, Divisheni ya makosa Rushwa na Uhujumu Uchumi leo imesomewa kielelezo cha kwanza cha ushahidi wa Jamhuri katika kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya ugaidi, inayomkabili kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu. Kielelezo hicho kimesomwa mbele ya Mahakama hiyo na ACP Ramadhani Kingai ambaye ni shahidi wa kwanza wa upande wa jamhuri katika kesi hiyo.

Akisoma kielelezo hicho ambacho ni maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Adam Kasekwa, ACP Kingai amedai yamechukuliwa katika Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Ilala (RCO), iliyopo katika Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, tarehe 7 Agosti 2020.

Kingai amedai, katika maelezo hayo mtuhumiwa huyo alidai alikwenda Moshi mkoani Kilimanjaro na wenzake, kwa ajili ya kazi ya ulinzi maalum wa mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na kwamba tarehe 25 Julai 2020, walipokelewa mkoani humo na wafanyakazi wa mwanasiasa huyo. Amedai, katika maelezo hayo Kasekwa alidai baada ya kupokelewa Moshi, walipelekwa katika Hoteli ya Aishi ambako walionana na Mbowe, ambaye aliwaeleza kwamba aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya anamsumbua, anatishia raia wa wilaya hiyo pamoja na kuwa na mpango wa kuiba kura.

Hivyo, hujuma za Sabaya zinampa wasiwasi yeye kupata ubunge na kuwa Mbowe aliwataka wamuwekee ulinzi Sabaya asifanikiwe. Akiendelea kusoma kielelezo hicho ACP Kingai  amedai, mtuhumiwa huyo alisema Mbowe aliwaelekeza wakamdhuru Sabaya kwa njia yoyote itakayowezekana ikiwemo kufuatilia nyendo zake katika maeneo anayopendelea kwenda hasa katika klabu za starehe Moshi na Arusha.

Kupita maelezo hayo ya onyo, mtuhumiwa alidai yeye na wenzake walipanga kumdhuru Sabaya kwa kutumia spray au perfume yenye sumu kwa kumwagia usoni. ACP Kingai aliendelea kusoma maelezo hayo ya onyo, yaliyodai kwamba Kasekwa alidai baada ya kupewa maelekezo hayo, walianza zoezi la ufuatiliaji nyendo za Sabaya katika klabu za starehe ikiwemo klabu kubwa ya Koko riko ya jijini Arusha, lakini hawakumkuta, hivyo yeye na wenzake walirudi jijini Dar ea Salaam, kuendelea na majukumu mengine waliyopangiwa.

Kwa mujibu wa kielelezo hicho Kasekwa na wenzake walienda Dar ea Salaam kuendelea na kazi nyeti, iliyodaiwa kuwa ni kulipua vituo vya mafuta, kukata miti , kuwadhuru viongozi wa Serikali na kufanya vurugu katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi, ili kuonesha Serikali imefeli kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2020.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted