Ethiopia yatangaza hali ya hatari waasi wa TPLF wakielekea Addis Ababa

Serikali ya Shirkisho imetangaza hali ya hatari itakayodumu kwa miezi sita huku Amerika ikiwataka waasi kutouteka mji wa Addis Ababa.

0

Maafisa katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa wamewataka wananchi kusajili silaha zao na kujitayarisha kulinda mitaa yao baada ya taarifa kuwa wapiganaji wa TPLF wanaelekea katika mji huo.

Agizo hili limetolewa siku kadhaa baada ya wapiganaji wa Chama cha Ukombozi cha Watu wa Tigray (TPLF) kudai kuiteka miji miwili ilioko umbali wa 400Km kutoka Addis Ababa.

Serikali ya Shirkisho imetangaza hali ya hatari itakayodumu kwa miezi sita huku Amerika ikiwataka waasi hao kutouteka mji wa Addis Ababa wenye idadi ya watu milioni tano.

“Nchi yetu inakabiliwa na hatari kubwa katika mamlaka yake na umoja, hatuwezi kuondoa hatari hii kupitia mifumo na taratibu za kawaida za kutekeleza sheria,” amesema Waziri wa masuala ya Haki Gedion Timothewos.

Mara ya mwisho Ethiopia ilitangaza hali ya hatari ilikuwa mwezi Februari 2018, hali ya hatari ilidumu kwa kipindi cha miezi sita wakati wa mabadiliko ya uongozi yaliyomleta Abiy Ahmed madarakani.

“Tunapinga mipango yoyote ya TPLF ya kutaka kuuteka mji wa Addis Ababa” amesema mjumbe maalum wa Marekani kwa Pembe ya Afrika Jeffrey Feltman.

Mapigano katika jimbo la kaskazini la Tigray yalizuka mwezi Novemba mwaka wa 2020 baada ya kikosi cha jeshi kilichokuwa wandani wa maafisa wa TPLF walipoteka kambi za majeshi katika eneo la kaskazini la Tigray, tukio hilo lilimsukuma Abiy kutuma majeshi Tigray.

Msemaji wa TPLF Getachew Reda amesema majeshi ya TPLF na wandani wake wakifaulu kuiondoa serikali, wataunda serikali ya mpito. “Kutakuwa na haja ya kuwepo kwa mazungumzo ya kitaifa,ila Abiy na mawaziri wake hawatashirikishwa bali watafikishwa mahakamani” amesema Reda.

Kufikia sasa wapiganaji wa TPLF wameiteka miji ya Amhara na Afar huku maelfu ya watu wakiuawawa na wengine zaidi ya milioni mbili wakitoroka makazi yao. Tangu kuzuka upya kwa mapigano, takriban watu 400,000 wameathirika na njaa kali.

Juhudi za kimataifa za kupata suluhu ya mapigano kati ya serikali na waasi, ambao awali walitofautiana kuhusu mageuzi ya kisiasa ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed yameambulia patupu. Mkuu wa ofisi ya amani na usalama ya Addis Ababa aliwapa wakazi siku mbili kusajili silaha zao au kuwapa jamaa wenye ozoefu wa kutumia silaha , kituo cha habari cha serikali Fana Broadcasting kilisema.

Kundi la waasi la TPLF linasema kuwa limeteka miji muhimu ya Dessie na Kombolcha na wanapanga kuelekea katika mji wa Kemise ulioko umbali wa 325Km kutoka mji mkuu wa Addis Ababa.

Waziri Mkuu Abiy Ahmed awali alikuwa amepuzilia mbali madai ya kutekwa kwa miji hiyo na kuwa wanajeshi wa nchi za kigeni wamekuwa wakishirikiana na TPLF, TPLF ilipinga madai hayo.

“Vita vinaweza kwenda usivyotarajia kwa sababu tofauti lakini mwishowe nchi itashinda vita vikuu” alisema Abiy Ahmed.

Kufikia jana jioni usafiri wa ndege ulikuwa haupatikani baada ya wanadiplomasia kuondoka Addis Ababa,wafanyakazi wa Ubalozi wa Amerika wanazuiwa kuondoka.

Waasi wa TPLF walitangaza kuuteka mji wa Kombolcha na Dessie siku ya Jumapili

Waziri mkuu Abiy Ahmed anawalaumu waasi kwa kuanza vita hivyo mwezi Novemba waliposhambulia kambi ya jeshi ya serikali ya shirikisho. Abiy kwa upande wake amekuwa akishtumiwa kwa kushirikiana na dikteta Afwerki kuanza vita Tigray na kukataa kufanya mazungumzo ya amani na TPLF.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted