Jaji Siyani awataka Naibu Wasajili kutimiza majukumu yao kikamilifu

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mustapher Siyani amewataka Naibu Wasajili kutimiza majukumu yao kikamilifu ili kuchochea maendeleo ya Mahakama.

0
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mustapher Siyani 

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mustapher Siyani amewataka Naibu Wasajili kutimiza majukumu yao kikamilifu ili kuchochea maendeleo ya Mahakama na utoaji haki kwa wananchi kwa wakati.

Jaji Siyani ameyasema hayo Novemba 25, 2021 wakati akiwaapisha Naibu Wasajili 27, katika ukumbi wa Mahakama Kuu jijini Dar es salaam

Siyani aliwafananisha wateule hao kama injini au moyo ambao ni muhimu katika kusukuma maendeleo yanatotakiwa kufanyika mahakamani.

“Mahakama itawategemea sana ninyi, kama Naibu Wasajili nitawafananisha na vitu viwili. Kama tunazungumzia chombo cha usafiri, ninyi ni injini au mashine inayowezesha chombo kile kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine, na kama nitawafananisha na viumbe hai ninyi ni moyo,” aliwaambia wateule hao.

Kwa mujibu wa Jaji Kiongozi, hakuna kati ya chombo cha usafiri au kiumbe hai ambacho kinachoweza kwenda sehemu moja kutoka sehemu nyingine kama injini au moyo haufanyi kazi. Hivyo, aliwataka viongozi hao kutimiza majukumu yao kikamilifu, kuwa  mfano wa uwajibikaji na kudhihirisha uwezo wao kwa kufanya kazi kwa bidii.

“Onyesheni kwamba baada ya miaka mingi  ambayo mmeitumikia Mahakama ya Tanzania sasa ni wakati mwafaka kwenu wa kuteuliwa kuwa Naibu Msajili na waliofanya uteuzi huo hawakukosea,” Jaji  Siyani alisema.

Jaji Kiongozi aliwahimiza Naibu Wasajili hao kwenda kusimamia uboreshaji wa huduma za Mahakama kwa vile wote wanafahamu uwelekeo ambao Mahakama ya Tanzania inakwenda kuwa Mahakama Mtandao.

“Kuweni madereva wa safari hiyo ya uboreshaji kuelekea Mahakama Mtandao. Mnajua miaka mitatu tangu sasa itakapofika 2025 tunapaswa kuondokana na matumizi ya karatasi. Teknolojia inapaswa kuwa ndiyo msingi wetu wa kufanya kazi na watakaosimamia au kuwa madereva wetu ni ninyi,” aliwaambia wateule hao.

Aidha, Jaji Kiongozi aliwakumbusha kuwa wanakwenda katika masjala mbalimbali, ambazo zina mashauri na baadhi ya masjala hizo zina mlundikano, hivyo wanawajibika kwa kushirikiana na Majaji na Mahakimu kuhakikisha Mahakama inaondokana na mlundikao au mashauri yanayokaa muda mrefu mahakamani.

“Hapa kuna dhana kwamba Msajili hana nafasi ya kusaidia kuondokana na mlundikano. Ukweli ni kwamba mipango yote itakayowezesha masjala moja kuondokana na mlundikano inaanzia kwa Naibu Msajili aliyepo kwenye masjala hiyo. Kwa hiyo, kama kutakuwa na Kanda au Mahakama ya chini ina mlundikano wa mashauri, mtu wa kwanza anayepaswa kutazamwa ni Naibu Msajili kwa sababu yeye ndiye msimamizi,” alisema.

Aliwakumbusha pia kurejea nyaraka mbalimbali zinazotolewa na Jaji Mkuu na ofisi ya Jaji Kiongozi ambazo zinatoa maelekezo mbalimbali ya namna wanavyotakiwa kutekeleza majukumu yao, hivyo aliwaonya kutokusherekea uteuzi walioupata kwa sababu kazi wanayokwenda kuifanya siyo nyepesi, hivyo wanapaswa kujiandaa kuchapa kazi.

Hata hivyo, Siyani aliwapongeza wote kwa uteuzi walioupata ambao umefuata na kuzingatia utendaji wao wa kazi na kwamba wote walioteuliwa walistahili na hapakuwa na upendeleo wowote. Aliwaambia kuwa wamepewa majukumu makubwa, hivyo Mahakama inategemea vingi kutoka kwao.

“Mmekula kiapo cha kuwa Naibu Msajili na  wote mlipitia usaili ambao unahusu, yanayotarajiwa kutoka kwenu kama Naibu Wasajili. Kwa kufaulu kwenu usaili ule, dhana iliyopo ni kwamba tayari wengi wenu mnafahamu majukumu yanayowakabili mbele yenu. Jukumu kubwa ni usimamisi wa Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufani na Mahakama zote. Nendeni mkasome majukumu ya Naibu Msajili ambayo yameaanishwa vizuri, myaelewe na kisha mkafanye kazi,” aliwaasa viongozi hao wa Mahakama.

Hafla ya uapisho huo ilihudhuriwa pia na Jaji Mkuu wa Tanzania,  Prof. Ibrahimu Hamis Juma, Majaji mbalimbali wa Mahakama Kuu ya Tanzania, akiwemo Jaji Mfawidhi Kanda ya Dar es Salaam, Amir Mruma, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Kelvin Mhina, Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Solanus Nyimbi , Wasajili na Watendaji mbalimbali kutoka Mahakama Kuu.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted