Mwanamume aliyefungwa jela kimakosa kwa miaka 42 afanyiwa mchango wa kiasi cha $1.6M kuanza maisha upya

Strickland aliwaambia polisi kuwa alikuwa nyumbani akitazama televisheni. Hakuna ushahidi wowote uliowahi kumhusisha na uhalifu huo.

0
Kevin Strickland

Kiwango cha fedha kilichochangishwa ili kumsaidia mwanamume wa Missouri nchini Amerika ambaye alitumikia kifungo cha zaidi ya miaka 42 jela kwa mauaji ya watu watatu ambayo hakufanya kimefikia $1.6M.

Kevin Strickland aliachiliwa Jumanne 23 Novemba akiwa na umri wa miaka 62. Strickland alikuwa amedumisha kutokuwa na hatia tangu kukamatwa kwake akiwa na umri wa miaka 18.

Kilikuwa kifungo kirefu zaidi katika historia ya jimbo hilo lakini chini ya sheria ya Missouri hana haki ya kupokea fidia yoyote ya kifedha hata baada ya kuhudumia kifungo cha miaka 42 kwa makosa ambayo hakutenda.

Kwa hivyo mawakili wake walizindua mchango unaojulikana kama GoFundMe kwenye mtandao ili kumsaidia katika gharama zake za maisha.

Kufikia Jumapili jioni, mchango ulikuwa umefika $1,511,440. Mawakili ambao walifanya kazi kwa miezi kadhaa kusaidia kumkomboa Bw Strickland, waliwasifu zaidi ya watu 27,000 ambao walimchangia fedha hizo.

Jimbo la Missouri huwalipa fidia tu wafungwa walioachiliwa huru kupitia ushahidi wa DNA, sio kwa sababu ya ushuhuda wa mashahidi, mawakili wake walisema.

Siku ya Jumanne 23 jaji aliamrisha kuachiliwa mara moja kwa Bw Strickland kutoka jela baada ya kuhudumia siku 15,487 gerezani.

Alihukumiwa kifungo cha maisha jela bila uwezekano wa kuachiliwa kwa miaka 50 baada ya kuhusishwa na uporaji wa nyumba katika Jiji la Kansas mnamo 25 Aprili 1978.

Usiku huo, washambuliaji wanne waliwapiga risasi watu watatu ndani ya nyumba hiyo: Sherrie Black, 22, Larry Ingram, 22, na John Walker, 20.

Mwathiriwa wa nne Cynthia Douglas, 20 alitoroka na majeraha baada ya kujifanya kuwa amekufa. Baada ya shinikizo kutoka kwa mpenzi wa dadake, polisi walimkamata kijana huyo Bw Strickland na kisha Bi Douglas akashinikizwa amtambue Strickland kutoka kwenye kundi la watu.

Bw Strickland aliwaambia polisi kwamba alikuwa nyumbani akitazama televisheni. Hakuna ushahidi wowote uliowahi kumhusisha na uhalifu huo.

Kesi yake ya kwanza mwaka wa 1979 iliisha bila hukumu kutolewa baada ya jaji mmoja mweusi kati ya majai 12 kutaka aachiliwe.

Katika kesi yake ya pili, majaji wote wazungu walimpata Bw Strickland na hatia ya kosa moja la mauaji na makosa mawili ya mauaji ya kiwango cha pili.

Miaka kadhaa baadaye, Bi Douglas alibadili ushuhuda wake akiandikia Mradi wa Innocence wa Midwest kwamba “mambo hayakuwa wazi wakati huo, lakini sasa najua zaidi na ningependa kumsaidia mtu huyu nikiweza.”

Bi Douglas alikufa kabla ya kubadili rasmi ushahidi wake dhidi ya Bw Strickland, lakini mama yake, dada yake na binti yake wote wametoa ushahidi mahakamani kwamba alimchagua “mtu ambaye siye.”

Waendesha mashtaka katika Kaunti ya Jackson walianza kukagua hukumu ya Bw Strickland Novemba mwaka jana na – chini ya sheria mpya ya Missouri – waliwasilisha ombi la kutaka kuachiliwa kwake mara moja.

Kevin Strickland
In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted