Rais Samia Suluhu, Oprah, Rihanna kwenye orodha ya Forbes ya wanawake wenye ushawishi mkubwa

Orodha hiyo ya Forbes inayojumuisha wanasiasa, watu mashuhuri na wanawake wafanyabiashara.

0
Rais wa Jamuhuri ya muungano ya Tanzania

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametajwa kwenye orodha ya Forbes ya wanawake wenye ushawishi mkubwa zaidi duniani kwa mwaka 2021.

Orodha hiyo ya Forbes inayojumuisha wanasiasa, watu mashuhuri na wanawake wafanyabiashara imekuwa ikiorodhesha wanawake wenye ushawishi mkubwa duniani kwa miaka 18 sasa.

Mwaka huu bilionea mfadhili MacKenzie Scott aliyekuwa mkewe bilionea Jeff Bezos, amechukua nafasi ya kwanza kwenye orodha.

Scott ni mwanamke wa tatu tajiri zaidi duniani, ufadhili wake wa miradi mingi ndio umemuweka katika nafasi ya kwanza.

Nyuma yake katika nambari ya pili ni makamu wa rais wa Amerika Kamala Harris, akiwa amepanda nafasi moja juu akibadilishana nafasi na Christine Lagarde, rais wa Benki Kuu ya Ulaya ambaye anashikilia nafasi ya tatu.

Mchapishaji wa jarida la Forbes amesema ingawaje watu walio katika orodha ya 18 ya “Wanawake 100 wenye ushawishi mkubwa duniani” ya mwaka 2021 wametoka kutoka nchi 18 na maeneo tofauti duniani na wanafanya kazi katika idara za fedha, teknolojia, siasa, uhisani, burudani na mengineyo wote wameunganishwa na suala la uwajibikaji.

Kwa mujibu wa mhariri wa jarida la Forbes, Maggie McGrath, Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amekuwa mstari wa mbele katika kuweka mikakati ya kukabiliana na kuenea kwa UVIKO 19 nchini mwake, na kwa juhudi zake ameorodheshwa kwa mara ya kwanza kwenye jarida hilo na anashikilia nafasi ya 94.

Orodha hiyo pia inajumuisha Rais wa Taiwan Tsai Ing-wen, ambaye mchango wake katika kuhakikisha uhuru na demokrasia nchini mwake licha ya shinikizo kutoka kwa Uchina kulimsogeza nafasi 28 mbele hadi kushikilia nambari Tisa. Wengine kwenye orodha hiyo ni mwanamke tajiri zaidi mweusi nchini Amerika na mmiliki wa kituo cha televisheni OWN, Oprah Winfrey, akiwa ameshikilia nafasi ya 23.

Oprah Winfrey

Msanii Rihanna kutoka Barbados anashikilia nafasi ya 68.

Kutoka nchini Nigeria, mwanzilishi na mmiliki wa kituo cha televisheni EbonyLife, Mo Abudu ameshikilia nafasi ya 98.

Msanii kutoka Amerika, Taylor Swift ameshikilia nafasi ya 78 na mwelekezi wa filamu kama vile “Salem” na “Queen Sugar” Ava Duvarney, akiwa katika nafasi ya 80.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted