Gavana wa kaunti ya Machakos, Kenya ndiye gavana bora zaidi barani Afrika

Tuzo ya Africa Illustrious, ilianzishwa mwaka wa 2020 na husimamiwa na My Media Africa.

0
Alfred Mutua, Gavana wa Machakos

Gavana wa Machakos Dkt Alfred Mutua ametuzwa kama “Gavana Bora kwa mwaka wa 2021”. Mutua alituzwa wakati wa toleo la pili la tamasha la kifahari la Africa Illustrious Award lililoandaliwa katika hoteli ya Radisson Blu mjini Lagos, Nigeria mnamo Alhamisi, Desemba 9, 2021.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mashuhuri kutoka bara zima la Afrika, maafisa wa serikali na wanahabari. Gavana Alfred Mutua aliandamana na Seneta wa Narok, Ledama Ole kina.

Gavana Mutua aliwapiku Oscar Mabuyane na Bushy Maape ambao ni Mawaziri wakuu wa jimbo la Eastern Cape na Kaskazini Magharibi kutoka Jamhuri ya Afrika Kusini. Viongozi hao watatu waliorodheshwa kuwania tuzo hiyo kwa sababu ya uongozi wao katika miundombinu, maendeleo ya vijana, kujenga vituo vya burudani na kuboresha huduma za afya.

Jopo hilo lilikubaliana kwa kauli moja kuhusu ushindi wa Dkt Mutua likitaja mafanikio yake kama Gavana wa Kaunti ya Machakos. Waliangazia vituo vya afya vilivyoko Machakos, haswa, kituo cha huduma na matibabu ya saratani bila malipo ambacho kinawahudumia Wakenya wanaougua saratani na pia kutaja ujenzi wa  barabara mpya za lami na maisha bora kwa wakaazi wa kaunti ya Machakos.

Prof. Henry Iwuanyanwu, mmoja wa wasimamizi wa hafla ya tuzo alisema kuwa “kaunti ya Machakos ni safi sana na inapendeza.”

Jopo hilo lilifurahishwa sana na sehemu ya burudani ya kipekee ya People’s Park huko Machakos, ambayo ni safi, nzuri na iliyo bure kwa Wakenya wote.

Pia walitaja ufadhili wa masomo unaotolewa kwa vijana, viwanja vya michezo miongoni mwa mengine. Prof. PLO Lumumba pia aliibuka kuwa “Pan-Africanist of all times.”

Viongozi wengine waliokuwa wakishindania tuzo hiyo ni pamoja na Emmanuel Tuloe kutoka Liberia, Mutebe Henry kutoka Uganda, Ousman Touray kutoka Gambia, Strive Masiyiwa kutoka Zimbabwe, David Adeleke (Davido) kutoka Nigeria, Mhe.Jewel Taylor, Makamu wa Rais wa Liberia, Chinedu Okoli (Flavour), Peter Ndifong kutoka Cameroon, Dk Charles Hackman kutoka Ghana, miongoni mwa wengine.

Tuzo ya Africa Illustrious, lilianzishwa mwaka wa 2020 na husimamiwa na My Media Africa, huwatambulisha na kuwasheherekea Waafrika mashuhuri ambao wamefanya vyema katika vitengo 36 tofauti vya shughuli za kuboresha maisha ya binadamu.

Vitengo hivyo ni pamoja na utawala, kilimo, elimu, sanaa, michezo, maendeleo ya jamii, uhisani, miongoni mwa mengine. Tuzo hiyo inatoa nafasi kwa viongozi kuteuliwa kutoka bara zima la Afrika na mataifa ya kigeni katika vitengo tofauti.

Baada ya hapo, umma kutoka kote barani Afrika unaalikwa kupiga kura kwa kutumia mitandao ya kijamii.

Orodha ya wale walioteuliwa inachunguzwa kwa kina na jopo la watu 26 mashuhuri kutoka kote barani ili kuwachagua washindi.

Mnamo 2020, Gavana Bora wa Mwaka alikuwa Babagana Umara Zulum, Gavana wa Jimbo la Borno nchini Nigeria.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted