Mtoto aliyepotea wakati wa kuhamishwa kwa maelfu ya wa Afghanistan aunganishwa na jamaa zake

Uwanja wa ndege wa Kabul ulivamiwa mwezi Agosti wakati maelfu ya watu walipokuwa wakihama kwenda Amerika baada ya majeshi ya Amerika kuondoka Afghanistan.

0

Mtoto aliyepotea wakati wa kuhamishwa kwa maelfu ya wa Afghanistan katika uwanja wa ndege wa Kabul ameunganishwa tena na jamaa zake baada ya miezi mitano, babu yake amesema.

Baba ya mvulana huyo alimkabidhi mtoto wake wa miezi miwili Sohail Ahmadi kwa mwanajeshi wa kigeni walipokuwa wakitoroka uongozi wa Taliban baada ya kundi hilo kuuteka mji mkuu Kabul katikati ya mwezi Agosti.

Wawili hao walitenganishwa, na kilichotokea baadaye hakijafahamika — lakini dereva wa teksi Hamid Safi alisema alimpata mtoto akilia akiwa peke yake katika uwanja wa ndege siku hiyo hiyo.

“Nilimpeleka kwa baadhi ya wanawake ili kumnyonyesha lakini hawakukubali… niliendelea kuitafuta familia yake,” alisema Safi ambaye alikuwa amekwenda uwanja wa ndege kumsaidia kakake kuhama.

“Nilimpigia simu mke wangu na akasema nimpeleke mtoto nyumbani.”

Wawili hao walisema waliendelea kuwatafuta wazazi wa mvulana huyo lakini waliposhindwa kuwapata, walimpa jina la Mohammad Abed na kuanza kumtunza.

“Kama hatungeipata familia yake basi tungemlinda na kumlea kama mtoto wetu, Safi, 29, aliiambia AFP.

Wakati huo huo, babake Sohail Mirza Ali Ahmadi alimtafuta kwa siku tatu kwenye uwanja wa ndege, hatimaye akaamua kupanda ndege kuelekea Amerika akiwa na mkewe na watoto wengine wanne.

Uwanja wa ndege wa Kabul ulivamiwa mwezi Agosti wakati makumi ya maelfu ya watu walipokuwa wakihama kwenda Amerika baada ya majeshi ya Amerika kuondoka Afghanistan baada ya miaka 20 ya vita.

Waafghanistan wengi walihofia kurejea kwa utawala wa Taliban wa miaka ya 1990 au kuadhibiwa kwa kushirikiana na Amerika au vikosi vya kigeni.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted