Waajiri wapewa siku saba kuwalipa wanahabari waliofariki kwenye ajali

Agizo hilo limetolewa leo wakati wa hafla ya kuaga na kutoa heshima za mwisho kwa waandishi watano na dereva wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza waliofariki...

0
Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amewapa siku 7 waajiri wanaodaiwa na waandishi wa habari waliofariki katika ajali ya agari wilayani Busega, kulipa stahiki zao marehemu hao na kutoa taarifa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mwanza.

Agizo hilo limetolewa leo wakati wa hafla ya kuaga na kutoa heshima za mwisho kwa waandishi watano na dereva wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza waliofariki dunia jana.

“Nimepewa salamu hapa kuwa miongoni mwa waliolala kwenye majeneza hapa mbele yangu hawajalipwa stahiki zao; natoa siku saba kwa waajiri wote wanaodaiwa kulipa stahiki zote za marehemu na kutoa taarifa ofisi ya mkuu wa mkoa,” ameagiza Nape

Akionyesha msisitizo kuhusu agizo hilo, Waziri huyo aliwataka wamiliki wa vyombo vya habari wanaodaiwa kutambua kwamba wizara yake ndiyo imeshikilia leseni zao.

“Yawezekana kuna hali ngumu ya kiuchumi, lakini nasema stahiki zote za marehemu hawa zilipwe ndani ya siku saba. Hayo ya hali ngumu tutayazungumza huko mbeleni kwa waandishi ambao wako hai ila kwa hawa marehemu lazima walipwe,” ameagiza Waziri Nape

Majeneza yaliyobeba miili ya waandishi wa habari watano waliofariki katika ajali wakiwa kwenye ziara ya mkuu wa mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel yakiwa yamewasili katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza kwa ajili ya shughuli ya kuagwa na ndugu, jamaa na marafiki. Picha na Mgongo Kaitira

Awali, wawakilishi wa waandishi wa habari waliotoa salamu walimuomba waziri huyo kushughulikia changamoto ya waandishi kutolipwa stahiki zao huku wakifichua kuwa baadhi ya marehemu hawajalipwa kwa miaka miwili iliyopita.

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC), Edwin Soko ndiye alikuwa wa kwanza kuiomba Serikali kuboresha sheria na mazingira ya kazi kwa waandishi wa habari kwa kuiomba wizara yenye dhamana kurekebisha kasoro zilizopo.

“Nitumie fursa hii kumwomba Waziri Nape Nnauye ambaye ndiye muasisi wa Sheria ya Huduna ya Habari ya mwaka 2016 kuwezesha waandishi wa habari kufanya kazi katika mazingira bora,” amesema Soko.

Katika hatua nyingine Waziri Nape Nnauye ameliagiza Jeshi la Polisi Nchini kuchambua matukio yote ya ajali za barabarani kwenye misafara ya Viongozi ambayo yamekuwa yakisababisha vifo vya Waandishi wa habari, ili kama kuna tatizo liweze kushughulikiwa.

Amewaeleza waombolezaji kuwa, Viongozi wa ngazi ya juu wamemuelekeza afuatilie matukio ya ajali za magari kwenye misafara ya Viongozi, ambapo mara nyingi waathirika ni Waandishi wa habari.

Waziri Nape amesema baada ya kukabidhiwa taarifa ya uchunguzi ndipo mambo mengine yatafuata ikiwemo kubadilisha utaratibu wa safari za Waandishi wa habari kwenye misafara ya Viongozi.

Kwa mujibu wa Waziri Nape, utaandaliwa utaratibu maalum au itifaki rasmi ya namna bora ya ushiriki wa Waandishi wa habari kwenye ziara hizo za Viongozi.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted