Rais Samia akerwa na wanaovujisha siri za Serikali

Asema suala la kutunza siri za Serikali limekuwa ni kama maradhi

0
Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Rais Samia Suluhu Hassan amewataka Mawaziri na Naibu Waziri, kutunza siri za Serikali, ili kuisaidia nchi katika gurudumu la maendeleo ambayo Serikali inafanya kwa ajili wa wananchi.

Rais Samia ameyasema hayo leo kwenye mkutano maalumu uliowakutanisha Mawaziri na Naibu Waziri katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, ambapo amebainisha kuwa suala la usiri wa nyaraka za serikali hivi sasa limekuwa tatizo kwani mara kadhaa kumeshuhudiwa kuvujishwa kwa taarifa huku wanaofanya michezo hiyo wakiwa ndani ya Serikali licha ya kuwa wamekula viapo.

“Suala la kutunza siri za Serikali limekuwa kama maradhi, unaweza kukuta hata nyaraka za Serikali kwenye mitandao, hili halipendezi na hakuna Serikali inayoendeshwa hivyo, nawahimiza mkalifanyie kazi suala la kudhibiti siri za Serikali” amesema Rais Samia.

Rais Samia pia amewataka mawaziri hao kuzingatia sheria, kanuni na taratibu huku akiwakumbusha viapo walivyokula wakati wa uapisho na kuwaambia kuwa viapo hivyo ni kwa ajili ya kwenda kuwatumikia wananchi.

Katika hatua nyingine Samia ameonekana kukasirishwa na hali ya migongano baina ya Waziri na Naibu wake katika utendaji kazi, haswa katika suala la nani atasafiri kwenda kufanya kazi fulani.

Ametaka migongano hiyo iachwe na waweke maslahi ya taifa kwanza kuliko maslahi yao binafsi.

“Nawaasa kuachana na migongano ya maslahi baina yenu kwani kila mmoja ana nafasi yake, ameaminika na kuteuliwa kufanya kazi” amesema Rais Samia na kuongeza 

“Masuala ya kufanya kazi kila mtu kivyake bila utaratibu mzuri ndani ya sekta au baina ya sekta na sekta sio sawa, katika kuyatimiza malengo ya kitaifa inatakiwa kuratibu na kufanya kazi kwa pamoja”

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted