Video ya mwanamke akicheza yachochea mjadala wa haki za wanawake nchini Misri

Baadhi ya wakosoaji wanamtuhumu kwa kukiuka maadili ya kihafidhina ya jamii ya Kiislamu huku wengine wakisimama kidete naye.

0

Video ya mama wa watoto watatu kutoka Misri ambayo ilisambaa mitandaoni na kumfanya mumewe ampe talaka na waajiri wake kumfukuza kazi imeibua mijadala mikali kuhusu haki za wanawake.

Video fupi ya simu ya rununu ya Aya Youssef, mwalimu wa shule ya msingi mwenye umri wa miaka 30, inamuonyesha akiwa amevaa hijabu, suruali na blausi ya mikono mirefu huku akicheza pamoja na wenzake, akitabasamu anapofurahia safari ya mtoni kwenye Mto Nile.

Lakini video hiyo, ambayo imesambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii tangu ilipochapishwa mapema mwezi huu, imezua maoni tofauti.

Baadhi ya wakosoaji wanamtuhumu kwa kukiuka maadili ya kihafidhina ya jamii ya Kiislamu — huku wengine wakisimama kidete naye.

Katika miaka ya hivi majuzi, Misri imeshuhudia visa kadhaa ambapo wanawake wamekuwa wakikabiliwa na kampeni za kukashifiwa kwenye mitandao ya kijamii, na kuibua hasira kwa waliohusika kuwajibika.

Haya yanajiri huku makundi ya kutetea haki za binadamu yakionya kuhusu kuenea kwa ukandamizaji wa uhuru katika taifa hilo la Afrika Kaskazini ambalo linazidi kuwa na wahafidhina tangu Rais Abdel Fattah al-Sisi aingie madarakani mwaka 2014.

Youssef, katika mahojiano ya hivi majuzi na chaneli ya kibinafsi ya TV, alisema alikuwa “mwenye furaha” kwenye safari hiyo.

Wenzake wengine walikuwa wakicheza pamoja naye kwenye mashua wengine wakipunga mikono hewani. “Sote tulikuwa tukicheza,” alisema.

Afutwa na kazi na kurudishwa

Lakini baada ya video hiyo kusambazwa mtandaoni, baadhi ya waliotazama walitoa maoni ya makali juu ya kile walichokiona kuwa tabia “isiyofaa”.

Mtumiaji mmoja wa Twitter, Jihad al-Qalyubi, alisema kitendo cha mwalimu huyo ni cha aibu.

Mwingine, Ahmed al-Beheiry, alisema “hakuweza kufahamu jinsi mwanamke aliyeolewa angecheza kwa njia hii chafu,”

Lakini — katika nchi ambayo asilimia 90 ya wanawake wenye umri wa kati ya miaka 18 na 39 waliripoti kunyanyaswa mwaka 2019, kulingana na utafiti wa mtandao wa utafiti wa Arab Barometer — wengine walimuunga mkono.

Baada ya video hiyo kusambaa, wizara ya elimu ya Misri katika eneo la Dakahlia — kaskazini mashariki mwa Cairo — ilimpeleka mwalimu huyo kwenye kamati ya nidhamu, na akafukuzwa kazi.

Baada ya kilio cha haki kutoka kwa watu wengi Misri na maeneo mengine dunaini alirejeshwa kazini wiki hii.

Nihad Abu al-Qumsan, mkuu wa Kituo cha Haki za Wanawake cha Misri, alimtetea mwalimu huyo na kumpa kazi.

“Tutauliza mahakama kuhusu sheria sahihi za densi — ili wanawake wote wafuate sheria zinazofaa ikiwa watacheza katika harusi za kaka zao au za watoto wao wa kiume, au siku za kuzaliwa,”Qumsan alisema kwa kejeli.

Ukweli kwamba mume wa Youssef pia alimtaliki baada ya kutazama video hiyo ulizua hasira kutoka kwa mwigizaji maarufu wa Misri Sumaya al-Khashab, akisema ilionyesha wazi kuwa wanawake na wanaume wamewekewa viwango tofauti na jamii.

“Kwanini wanaume hawawasamehe wake zao baada ya matukio kama haya,” Khashab aliuliza.

“Kuna wanawake wengi wanaosimama na wanaume wao wanapokwenda gerezani, kwa mfano, au kutowatelekeza waume zao hali zao zinapokuwa mbaya,” aliongeza.

Youssef aliliambia gazeti la Al-Watan la Misri kwamba hakujua ni nani aliyechapisha video hiyo mtandaoni, lakini aliapa kuwachukulia hatua za kisheria wale ambao “walimharibia sifa na kuharibu nyumba yake.”

Si kisa cha kwanza kama hiki cha aibu mtandaoni kuzua hasira nchini Misri.

Vijana wawili walikamatwa wiki hii baada ya msichana wa shule mwenye umri wa miaka 17 kujiua mwezi uliopita.

Alimeza sumu baada ya kudaiwa kunaswa kwa picha zilizobadilishwa kidijitali baada ya kuripotiwa kukataa kuwa na uhusiano wa kimapenzi nao.

Na mnamo Julai 2021, mahakama ya Cairo iliwahukumu wanawake wawili kifungo cha miaka sita na 10 jela kwa “kukiuka maadili ya umma” baada ya kuchapisha video kwenye mtandao wa kijamii TikTok.

Walikuwa miongoni mwa “washawishi” kadhaa wa mitandao ya kijamii waliokamatwa mwaka 2020 kwa “kukosa maadili ya jamii” nchini Misri.

Misri imechukuliwa kwa muda mrefu kama mahali pa kuzaliwa kwa densi aina ya “belly dance”, lakini wacheza densi kadhaa wa tumbo na waimbaji wa pop wamekuwa wakilengwa katika miaka ya hivi majuzi kutokana na maudhui ya mtandaoni yanayochukuliwa kuwa ya kinyama au ya kuchukiza.

Misri imeshuhudia wacheza densi kutoka nchini humo ikipungua, kwa kiasi kikubwa kutokana na sifa mbaya ya taaluma hiyo kwani nchi hiyo imekuwa ya kihafidhina zaidi katika kipindi cha nusu karne iliyopita — na kwa ukandamizaji mkubwa wa uhuru.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted