Nyuma ya pazia kuhusu soko la Karume ilivyowafanya wamachinga kuandamana

Wadai kupata taarifa kuwa eneo la soko hilo liko mbioni kukodishwa kwa mwekezaji

0
Soko la Karume lawaka moto

Wakati bado wafanyabiashara wa soko la Karume wakiendelea kubaki katika alama ya kuuliza na kutokujua nini cha kufanya baada ya kuingia hasara iliyotokana na moto kuwaka katika soko ambalo wamekuwa wakifanya biashara zao za kila siku, zimeibuka tetesi kuwa huenda huo ulikua ni mpango wa kuwahamisha wamachinga ili kupisha muwekezaji katika eneo la soko hilo.

Mapema leo asubuhi wafanyabiashara wadogo katika soko hilo waliandamana hadi katika ofisi za mkuu wa mkoa wa Dar es saaam bwana Amosi Makala wakimshinikiza kutoa tamko la kuwaruhusu waendelee kufanya biashara wakati huu ambapo serikali inaendelea kufanya uchunguzi na hii ni baada ya wafanyabiashara hao kukosa imani na matamko ya viongozi wa serikali kuhusu jambo hilo.

Hata hivyo hiyo ilikua ni miongoni mwa sababu zilizowafanya wamachinga hao kuandamana lakini pia katika nyakati tofauti wameibua hoja nzito ya kwamba walisikia kuwa eneo hilo la soko liko katika mpango wa kupewa mwekezaji jambo ambalo lilwafanya kuwa na hofu, wakihofia kupoteza haki zao na ndio wakaona ni bora waandamane.

Msemaji wa wafanyabiashara hao bwana Ismail Feisal amesema mwanzo walifanya maandamano ya Amani baada ya kupata taarifa kuwa Serikali inataka kukodisha eneo hilo 

“Unajua mwanzo tulifanya maandamano ya amani tulikosa imani na maagizo yao baada ya kupata taarifa Serikali inataka kukodisha eneo hili kwa muwekezaji tuliona haki yetu inaweza kupoteza,” amesema Feisal

Hata hivyo tetesi hizo zimepatiwa majibu baada ya kufanyika kikao kati ya viongozi wanaowawakilisha wafanyabiashara hao na Mkuu wa wilaya ya Ilala Ng’wilabuzu Ludigija, na kusema kuwa hakukuwa na mpango wowote baina ya soko hilo na Serikali kuhusu kumuweka muwekezaji.

Mkuu wa Wilaya amewaahidi kuwa baada ya siku saba  zilizotolewa  na Serikali kufanya uchunguzi zikipita, wafanyabishara hao wataruhusiwa kuanza kujenga mabanda yao na kuendelea na shughuli zao.

Kwa sasa wafanyabiashara hao wameruhusiwa kuweka alama kwenye maeneo yao ili wajihakikishie usalama wakati wakisubiria ripoti ya kamati iliyoundwa kuchunguza chanzo cha moto uliosababisha kuteketea kwa soko hilo.

“Tunashukuru tumekubaliana na Serikali kwamba tuweke alama wakati kamati ikiendelea kuchunguza kubaini chanzo”- amesema Mfanyabiashara wa Wafanyabiashara ndogondogo Ismail Feisal.

Jana Jumapili baada ya soko hilo kuungua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Amos Makalla aliagiza wafanyabiashara hao kusitisha shughuli zote katika eneo hilo mpaka kamati ya uchunguzi itakapokamilisha kuchunguza.

Itakumbukwa kuwa hii ni mara ya tatu kwa soko hilo lenye zaidi ya wafanyabiashara 3500,  kuungua moto ambapo inadaiwa kuwa asilimia 98 ya mali za wafanyabiashara hao zimeteketea kwa moto 

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted