Vikosi vya usalama Sudan vyawaua waandamanaji saba katika maandamano ya kupinga mapinduzi

Vifo hivyo saba vinafikisha 71 idadi ya waandamanaji waliouawa tangu jeshi lilipochukua madaraka Oktoba 25, likiongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.

0

Vikosi vya Sudan viliwafyatulia risasi waandamanaji saba Jumatatu katika moja ya maandamano mabaya zaidi ya hivi punde dhidi ya mapinduzi ya kijeshi, huku wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakiitaka Khartoum kuepuka kutumia nguvu kupita kiasi.

Ghasia za hivi punde, zilizotokea katika mji mkuu na katika miji mingine mikubwa, zikiwa zinakuja kabla ya ziara kuu ya wanadiplomasia wa Amerika, huku Washington ikitaka kukomeshwa kwa mzozo huo uliodumu kwa miezi kadhaa katika taifa hilo la kaskazini mashariki mwa Afrika.

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa Volker Perthes alivishtumu vikosi vya usalama “kwa kuendelea kutumia risasi za moto,” wanapokabiliana na waandamanaji, na kuthibitisha kuwa takriban watu saba wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa, huku ubalozi wa Amerika mjini Khartoum ukikosoa “mbinu wanazotumia vikosi vya usalama vya Sudan.”

Wanachama tisa wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zikiwemo Uingereza na Ufaransa walizitaka pande zote “kujiepusha na matumizi ya ghasia ili kuwasilisha ujumbe wao,” wakisisitiza umuhimu wa “kukusanyika kwa amani na uhuru wa kujieleza.”

Vifo hivyo saba vilivyotokea Jumatatu vinafikisha 71 idadi ya waandamanaji waliouawa tangu jeshi lilipochukua madaraka Oktoba 25, likiongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.

Unyakuzi huo wa kijeshi ulizua shutuma za kimataifa, na ulivuruga mchakato wa serikali ya mpito uliostahili kurejesha utawala wa kiraia kufuatia kuondolewa madarakani kwa rais wa muda mrefu wa kiimla Omar al-Bashir Aprili 2019.

Waandamanaji — wakati mwingine wakiwa makumi kwa maelfu — wamejitokeza mara kwa mara mitaani licha ya vikosi vya usalama kubana mawasiliano mara kwa mara tangu mapinduzi.

Siku ya Jumatatu, madaktari wanaopinga mapinduzi walisema waandamanaji watatu walipigwa risasi huku kamati Kuu huru ya Madaktari wa Sudan ikiripoti kuwa wengine wanne waliuawa wakati wa “mauaji yaliyotekelezwa na mamlaka ya mapinduzi.”

Madaktari waliripoti kuwa wengi walijeruhiwa na risasi za moto.

Muungano wa kiraia wa Sudan, Forces for Freedom and Change, ulitoa wito kwa raia kuandamana kufuatia mauaji yaliyotelekezwa na vikosi vya usalama.

Maafisa wa usalama walifyatua risasi na vitoza machozi kuwalenga waandamanaji waliotoka kutoka miji ya Khartoum, na kitongoji cha Kaskazini cha Khartoum na mji wa Omdurman katika mto Nile.

Watu kadhaa walionekana wakiwa na shida  kupumua na wengine wakivuja damu kutokana na majeraha ya vitoa machozi, mwandishi wa AFP alisema.

Waandamanaji walitumia mawe na kuchoma moto matairi kutengeneza vizuizi barabarani, wakiwataka wanajeshi warudi kwenye kambi zao, na kuimba nyimbo za kuunga mkono utawala wa kiraia, mashuhuda walisema.

Ilipofika usiku, mamia ya waandamanaji walibaki mitaani katika maeneo kadhaa ya Khartoum, huku wanaharakati wanaounga mkono demokrasia wakiongoza miito ya mtandaoni kuendelea na maandamano hayo.

Mamlaka imekanusha mara kwa mara kutumia risasi za moto katika kukabiliana na waandamanaji, na kusisitiza kuwa maafisa wengi wa usalama wamejeruhiwa wakati wa maandamano, akiwemo jenerali wa polisi aliyechomwa kisu hadi kufa wiki jana.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted