Mkinichagua kuwa rais nitahalalisha bangi na kupunguza siku rasmi za kufanya kazi; Muaniaji urais Kenya

Kulingana na Wajackoyah, uuzaji wa bangi katika masoko ya nje kutasaidia kupunguza madeni ya kitaifa na hivyo kupunguza mzigo wa deni na nchi ya China

0
Prof. George Wajackoyah, muaniaji wa kiti cha Rais

Uchaguzi mkuu nchini Kenya unatarajiwa kufanyika mnamo Agosti 9 2022.

Wanasiasa na watu tofauti wamejitokeza kuwania nyadhfa tofauti ikiwemo ugavana, useneta na hata rais. Kati ya wale ambao wameweka wazi azma yao ya kuwania kiti cha urais ni aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga wa muungano wa Azimio la Umoja na Naibu wa Rais William Ruto kutoka muungano wa Kenya Kwanza.

Kunaye mgombezi mwingine ambaye pia amejitosa katika kinyang’anyiro hicho kwa mara ya pili na ni Profesa George Wajackoyah, aliyetangaza azma yake ya kuwania kiti cha urais mara ya kwanza mwaka wa 2013 ila baadae akajitoa kinyang’anyironi.

Katika uzinduzi wa manifesto yake, Wajackoyah alikuwa na ahadi nyingi kwa wakenya iwapo watamchagua kuwa rais wa tano wa taifa hilo.

Kati ya ahadi hizo ni kuhalalalisha upandaji na uvutaji wa bangi,kuwa na mawaziri wakuu wanane , matibabu ya bure kwa watoto, wazee na wanawake wajawazito.

Kulingana na Wajackoyah, uuzaji wa bangi katika masoko ya nje kutasaidia kupunguza madeni ya kitaifa na hivyo kupunguza mzigo wa deni na nchi ya China, aliongeza kuwa watu wanaovuta bangi huishi kwa miaka mingi.

Afadi nyingine alizotoa kwa wakenya iwapo watamchagua kuwa rais na kumrithi Uhuru Kenyatta ni kuwa, atapunguza siku za kufanya kazi ziwe nne, wakenya wafanye kazi kuanzia Jumatatu hadi Alhamis pekee,akisema hii itawapa fursa watu wa dini ya kiislamu kufanya swala Ijumaa bila usumbufu, na wakristo nao kutoka madhehebu tofauti kuabudu Jumamosi na Jumapili.

Kando na kuwa yeye ni profesa, George Wajackoyah ni wakili mwenye tajriba ya miaka mingi. Katika uzinduzi wa manifesto yake siku ya Jumamosi 12 Februari katika hoteli ya Diamond Plaza jijini Nairobi, alitangaza kuwa atawania kiti cha urais kupitia chama cha Roots Party of Kenya.

Kuhusu maendeleo ya miundombinu, profesa alipendekeza kuondolewa  kwa mji mkuu kutoka Nairobi hadi jiji jingine tofauti.

Wajackoyah alisema utawala wake utaanzisha hukumu ya kifo kwa watu wafisadi na kuongeza kuwa mara tu atakapoingia mamlakani, katika muda wa miezi sita ya kwanza, atasimamisha Katiba ili kuruhusu Wakenya kuamua aina ya Katiba wanayoitaka.

Kumhusu George Wajackoyah

George Wajackoyah ana umri wa miaka 62 na ni mzaliwa wa magahribi mwa Kenya. Alijipata jijini Nairobi baada ya kutelekezwa na wazazi wake alipokuwa na umri wa miaka 16, akaambulia kuwa mtoto wa mitaani.

Alipata kuokolewa na msamaria mwema aliyemchukua na kumpeleka shule alikosoma hadi kidato cha sita.

Baada ya kuhitimisha masomo yake, alijiunga na chuo cha polisi na baadae akawa polisi hadi kuja kupandishwa cheo na kuwa inspekta.Mwaka wa 1990 alihamia Uingereza alikosomea uwakili akipata karo ya shule kwa kuchimba makaburi.

Wajackoyah ana shahada ya uanasheria  LLB (Hons) kutoka Chuo Kikuu cha Wolverhampton (Uingereza), shahada ya CCL/LLM, Shule ya Mafunzo ya Mashariki na Afrika, Chuo Kikuu cha London, Chuo Kikuu cha LLM cha Warwick (Uingereza), Chuo Kikuu cha LLM cha Baltimore, na Diploma ya Juu ya lugha ya Kifaransa kutoka Chuo Kikuu cha Burundi.

Yeye ndiye mshirika mwanzilishi wa ofisi ya wanasheria ya  Luchiri & Co. Advocates na kwa sasa ni Mwanachama wa Kitivo katika Taasisi ya Uhamiaji katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted