Amuua mke kisha amzika kwenye shamba

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, ACP Nicodemus Katembo, amesema tukio hilo limetokea Februari 28, mwaka huu, katika kijiji cha Lipalwe mkoani Mtwara

0

Jeshi la Polisi mkoani Mtwara linamtafuta Shahibu Kuselela ambaye anadaiwa  kumuua mke wake kwa kitu chenye ncha kali na baadae kumzika kwenye shamba na kisha kupanda mpunga ili kupoteza ushahidi

Akizungumza na wanahabari mkoani hapo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, ACP Nicodemus Katembo, amesema tukio hilo limetokea Februari 28, mwaka huu, katika kijiji cha Lipalwe mkoani Mtwara.

Alisema kuwa mwanamume huyo alifanya unyama wa mauaji hayo ya mkewe Amina Mtausi (40) kwa kutumia kitu kinachodaiwa kuwa na ncha kali.

Alieleza baada ya kutekeleza mauaji hayo aliuchukua mwili wa marehemu na kwenda kuufukia katika shimo shambani kwao kisha kuchukua mpunga na kuupanda juu ya shimo hilo.

Pia, baada ya kutekeleza azma yake alitoweka kusiko kujulikana kutokana na kuhofia kukamatwa na vyombo vya sheria na chanzo cha mauaji hayo hakijajulikana.

ACP Katembo alisema tukio hilo limegundulika juzi baada ya mdogo wa mtuhumiwa huyo, Omari Saidi, alipokuwa akienda kisimani kuchota maji katika shamba hilo na kubaini harufu isiyo ya kawaida.

Alisema alipofuatilia kujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kikitoa harufu aliona baadhi ya viungo vya marehemu huku sehemu ya mwili ukiwa umefukiwa ndani ya shimo.

ACP Katembo alisema, Saidi alitoa taarifa kwa vyombo husika kwa ajili ya kufuatilia tukio hilo kwa kina zaidi.

Jeshi la Polisi mkoani Mtwara lilifika katika eneo hilo la tukio wakiambatana na madaktari kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu wa mwili huo na hatimaye baada ya vipimo ulibainika kuwa na majeraha ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali sehemu za kisogoni na kutokwa na damu iliyosababisha kupoteza maisha.

Jeshi la Polisi bado linaendelea kumsaka mtuhumiwa huyo ili afikishwe katika mahakama kwa ajili ya kujibu tuhuma zinazomkabili za mauaji.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted