Morocco: Makumi wafa maji baada ya mashua yao kupinduka wakihamia Uhispania

Takriban wahamiaji 44, wakiwemo wanawake na watoto wachanga, walikufa maji wiki hii kwenye pwani ya Morocco walipokuwa wakijaribu kufika Uhispania

0

Takriban wahamiaji 44, wakiwemo wanawake na watoto wachanga, walikufa maji wiki hii kwenye pwani ya Morocco walipokuwa wakijaribu kufika Uhispania, shirika la misaada la wahamiaji Caminando Fronteras limesema.

Ikinukuu jamaa za waathiriwa, ilisema miili ya wanawake watano na watoto wawili ilifikishwa ufukweni lakini waliosalia bado hawajapatikana.

“Janga kubwa. Takriban waathiriwa 44 walikufa maji kwenye ufuo wa Tarfaya (kusini mwa Morocco),” Helena Maleno wa shirika hilo la usaidizi alitweet Jumamosi.

Walikuwa miongoni mwa wahamiaji 61 ambao walipanda mashua kuelekea Visiwa vya Canary vya Uhispania, karibu kilomita 100 kutoka Tarfaya, alisema.

Jumla ya wanawake 16 na watoto wachanga sita walikuwa miongoni mwa waliokuwemo kwenye mashua, Maleno alisema.

“Miili ya wanawake watatu na watoto wawili sasa iko katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Laayoune,” jiji kuu katika eneo linalozozaniwa la Sahara Magharibi.

Ufalme wa Afrika Kaskazini wa Morocco ni kitovu muhimu cha kupita kwenye njia zinazochukuliwa na wahamiaji wanaotarajia maisha bora barani Uropa.

Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya ndani ya Uhispania, zaidi ya wahamiaji 40,000 waliwasili nchini kwa njia ya bahari mwaka 2021. Umoja wa Ulaya ulisema wiki hii ulitaka kuimarisha ushirikiano na Morocco ili kukomesha wimbi la wahamiaji haramu wanaoingia katika Umoja huo, huku kukiwa na ongezeko kubwa la watu wanajaribu kufikia Visiwa vya Canary — lango la EU.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted