LHRC yalaani tukio la askari aliyemuaa raia huko Kigoma nchini Tanzania

Katika taarifa iliyotolewa leo na LHRC, imeeleza kwamba Pamoja na mamlaka waliyopewa Jeshi la Polisi ya kutuliza ghasia, bado jeshi hilo linawajibika kuheshimu, kuzingatia na kulinda misingi, kanuni,...

0

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimelaani tukio la mauaji ya Bw. Juma Ramadhan (35), kwa kupigwa risasi wakati jeshi la polisi mkoani Kigoma likijaribu kudhibiti vurugu, Machi 14, 2022 katika uwanja wa Lake Tanganyika- Kigoma.

Jana Machi 15, Jeshi la Polisi lilitoa taarifa kwamba Askari polisi mwenye namba F.5123 D/ CPL Subira ambaye aliyekuwa na bunduki aina ya AK 47 adaiwa kumuua Juma Ramadhani kwa kumpiga risasi na kuwajeruhi watatu wakati akiwa kwenye harakati za kujihami kwenye vurugu zilizotokea katika kiwanja cha mpira cha Lake Tanganyika mkoani Kigoma, nchini Tanzania.

Katika taarifa iliyotolewa leo na LHRC, imeeleza kwamba Pamoja na mamlaka waliyopewa Jeshi la Polisi ya kutuliza ghasia, bado jeshi hilo linawajibika kuheshimu, kuzingatia na kulinda misingi, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali  ya utendaji kazi wa Jeshi hilo ikiwemo Mikataba wa Umoja wa Mataifa wa Matumizi ya Nguvu na Silaha wa mwaka 1990, pamoja na Mwongozo wa Utendaji kazi wa Jeshi la Polisi(PGO Marejeo ya mwaka 2021.)

“Kituo cha sheria na Haki za Binadamu, kinasikitishwa na muendelezo wa matukio yanayoendelea  yanayolihusu Jeshi la Polisi” Imesema taarifa hiyo.

Tukio hilo limetokea ikiwa ni siku chache tu tangu Katibu mwenezi wa CCM kutoa malalamiko juu ya mwenendo wa Jeshi la Polisi, mbele ya vyombo vya habari aliyetaka kuundwa kwa tume maalum kuchunguza mwenendo wa jeshi hilo

Itakumbukwa pia ni hivi karibuni tu Waziri Mkuu Kassim Majliwa aliunda Kamati ya Uchunguzi dhidi ya Mauaji ya mfanyabiashara  wa madini mkoani Mwara yaliyotokea mnamo Februari, 2022.

Kutokana na msululu wa visa vya polisi kuwafanyia ukatili raia LHRC, imeitaka Serikali, kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya maafisa wa polisi waliohusika katika tukio hilo, lakini pia kuundwa Tume huru ya kijaji itakayofanya uchunguzi juu ya utata wa kifo cha bwana Juma Ramadhani na kuanzisha chombo huru maalum kwa ajili ya kupokea na kuchunguza malalamiko dhidi ya jeshi la polisi nchini.

Polisi nchini Tanzania wamekuwa wakilalamikiwa mara kwa mara na wananchi kutokana na matendo yao maovu wanayoyafanya kinyume na sheria, na hata kuwabambikia kesi wananchi wasio kuwa na hatia.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted