Watu 17 wanakabiliwa na mashtaka ya kujaribu kuua kwa kushambulia helikopta ya Raila Odinga

Watu hao17 wanahusishwa na kisa cha machafuko ambapo helikopta iliyokuwa imembeba Odinga ilipigwa mawe

0

Washukiwa 17 wamefikishwa mahakamani mjini Eldoret kuhusiana na shambulizi la Ijumaa dhidi ya kinara wa ODM na anayewania kiti cha urais kupitia Muungano wa One Kenya Alliance Raila Odinga katika eneo la Kabenes, Kaunti ya Uasin Gishu.

Watu hao 17 wanahusishwa na kisa cha machafuko ambapo helikopta iliyokuwa imembeba kiongozi wa ODM ilipigwa mawe katika mazishi ya Mzee Jackson Kibor.

Hakimu Mkazi Mkuu Emily Kigen aliamuru wazuiliwe katika kituo cha polisi cha Eldoret ili kuwezesha DCI kukamilisha uchunguzi dhidi yao.

Washukiwa hao wamefunguliwa mashtaka kwa makosa ya kujaribu kuua, kuharibu mali na kusababisha vurugu.

Upande wa mashtaka,ulipendekeza washukiwa hao wazuiliwe rumande kwa siku 14 ili kuruhusu polisi kukamilisha uchunguzi.

Washukiwa  waliofikishwa mahakamani ni pamoja na Abednego Kiptanui, Godwin Kipchirchir, Abraham Chemja, Rodgers Kiplimo, Sammy Keter, Elvis Kipkoech, Moses Bahati, Edwin Cheruiyot, William Samal Erupe, Cleophas Cheboi, Peris Maiyo, Elias Kiplagat, Eliud Kimelimba Kiplaga, , Kenneth Sawe, Kipkorir Muge na Collins Cheboi.

Mwendesha mashtaka aliambia mahakama kuwa washukiwa waliharibu helikopta ambayo thamani yake inazidi KSh300 milioni.

Jumamosi jioni, Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ,DCI alisema kuwa uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa ghasia hizo zilipangwa na kuratibiwa na Mbunge wa Soi Caleb Kositany pamoja na mwenzake wa Kapseret Oscar Sudi na Spika wa Bunge la Kaunti ya Uasin Gishu David Kiplagat, ambao waliitwa kuhojiwa katika makao makuu ya DCI ya Rift Valley, mjini Nakuru siku ya Jumapili.

Kulingana na DCI katika ripoti yake ya awali, vijana waliorushia mawe msafara wa Bw Odinga, ikiwa ni pamoja na helikopta yake, walichochewa.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted