Kenya: Uteuzi wa wagombea viti katika chama cha UDA wafanyika

Wakati Uchaguzi Mkuu unapokaribia, vyama vya siasa vinaharakisha kukamilisha mchujo wa vyama vyao kabla muda wa makataa Aprili 22,2022

0

Uteuzi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) ulianza Alhamisi, Aprili 14, katika kaunti 36 huku viongozi hao wakiwahakikishia wanaowania kuwa mchakato huo utakuwa huru na wa haki.

UDA itatumia kura za mchujo kuwachagua wagombeaji watakaochuana na wagombea wengine kutoka miungano mingine katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Katika taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB), Anthony Mwaura, chama hicho kimetenga vituo 15,000, masanduku 75,000, wasimamizi wa uchaguzi wa kaunti 47 na wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo 200 kusimamia mchakato mzima.

Aidha, imetuma maafisa wasimamizi 21,000 na makarani 52,000.

Kati ya maeneo ambako kura ya uteuzi umeahirishwa ni:

Zoezi la uteuzi wa UDA katika Milima Elgon na Kakamega umeahirishwa hadi Ijumaa, Aprili 15.

Upigaji kura umesitishwa katika eneo la Baringo ya Kati baada ya vituo 22 vya kupigia kura kuripoti ukosefu wa rejista za wanachama wa UDA, kura ya mchujo Turkana imeahirishwa hadi Aprili 19.

Wawaniaji wa kiti cha ugavana wa UDA ambao wameteuliwa bila kupingwa ni pamoja na: aliyekuwa seneta wa Mombasa Hassan Omar anayewania ugavana kaunti ya Mombasa, Fatuma Mohamed Achani wa Kwale, mbunge wa sasa wa Malindi Aisha Jumwa anayewania ugavana kaunti ya Kilifi, Tuneya Hussein Dado wa Tana River, Alice Wahome wa ambaye ndio mbunge wa sasa wa Kandara, John Mtuta wa Taita Taveta na Mohamed Barrow wa Garissa.

UDA ilipuzilia mbali ripoti za kuwepo kwa karatasi ghushi za kupigia kura.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi ya UDA (NEB), Anthony Mwaura, alishikilia kuwa hakukuwa na karatasi ghushi na uchunguzi kuhusu suala hilo unaendelea.

Aliongeza kuwa chama hicho kimechapisha karatasi za kupigia kura za kipekee ambazo haziwezi kuigwa wala kuzalishwa kwa wingi popote.

Wakati Uchaguzi Mkuu unapokaribia, vyama vya siasa vinaharakisha kukamilisha mchujo wa vyama vyao kabla muda wa makataa Aprili 22, 2022.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted