Hukumu katika kesi ya Uhujumu Uchumi inayomkabili Sabaya na wenzake kutolewa leo

Awali, Mei 31 mwaka huu Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Patricia Kisinda aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo, alipanga kutoa hukumu lakini ilishindikana kutokana na kudaiwa kuwa nje ya...

0

Hatima ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi inatarajiwa kujulikana leo.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha iliyokuwa ikisikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 27/2021 imepanga kwa mara ya pili kutoa hukumu hiyo.

Awali, Mei 31 mwaka huu Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Patricia Kisinda aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo, alipanga kutoa hukumu lakini ilishindikana kutokana na kudaiwa kuwa nje ya kituo cha kazi kwa majukumu mengine.

Sabaya na wenzake walikuwa wakisubiri hukumu hiyo endapo wangeachiwa huru au la, kabla ya kufunguliwa kesi nyingine na wenzake watano ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Juni Mosi mwaka huu.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Fadhil Mbelwa akiahirisha kesi hiyo Mei 31 mwaka huu alisema hakimu aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo amepangiwa majukumu mengine nje ya kituo cha kazi hivyo hukumu hiyo itatolewa leo.

Hukumu hiyo inatarajiwa kutolewa baada ya kesi hiyo kusikilizwa kwa miezi saba tangu ilipoanza Julai, 2021.

Katika kesi ya kwanza walihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, hukumu ambayo Mei 6, 2022 ilitenguliwa na Mahakama Kuu na kuwaachia huru baada ya kubaini dosari.

Washitakwa wengine katika kesi hiyo ni Enock Mnkeni (41), Watson Mwahomange (27), John Aweyo (45), Syliverster Nyegu (26), Jackson Macha (29) na Nathan Msuya (31).

Mashitaka matano yanayowakabili washtakiwa hao ni uhujumu uchumi, utakatishaji fedha, kuongoza genge la uhalifu, kuomba rushwa ya Sh milioni 90 na kutumia madaraka vibaya.

Sabaya na wenzake walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Juni 4, mwaka jana na kesi yao ilianza kusikilizwa Oktoba, mwaka jana.

Upande wa Jamhuri unaongozwa na Mwendesha Mashitaka Mwandamizi wa Serikali, Felix Kwetukia akisaidiwa na Mwendesha Mashitaka Mwandamizi, Tasila Asenga, Ofmed Mtenga, Neema Mbwana na Richard Jacopiyo ambaye ni Wakili wa Takukuru.

Upande huo ulikuwa na mashahidi 13 na vielelezo tisa na upande wa utetezi ulipeleka mashahidi nane.

Wakili Mosses Mahuna anaongoza jopo la mawakili wa upande wa utetezi akisaidiwa na Faudhia Mustapher, Edmund Ngemela, Fridorini Bwemelo na Sylivester Kahunduka.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted