Msafara wa Rais wa Nigeria washambuliwa na watu wasiojulikana.

Shambulio hilo linadhihirisha kuwa hali ya usalama nchini Nigeria ni mbaya kutokana na makundi ya uhalifu yanazuka kila uchwao

0
Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari

Watu wenye silaha wameshambulia msafara wa Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari kabla kiongozi huyo kuanza  ziara yake katika jimbo lake la kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Buhari hakuwa kwenye msafara huo wakati watu wenye silaha walipovamia magari ambapo taarifa zinaeleza kuwa  watu wawili walijeruhiwa.

Shambulio hilo linadhihirisha kuwa hali ya usalama nchini Nigeria ni mbaya kutokana na makundi ya uhalifu yanazuka kila uchwao

Buhari anatarajiwa kuzuru mji aliozaliwa wa Daura katika Jimbo la Katsina mwishoni mwa juma kwa ajili ya kusheherekea sikukuu ya Eid-ul-Adha ambayo inategemewa kuwa Julai 10 siku ya Jumapili.

Watu wenye silaha walifyatua risasi karibu na Daura kwenye msafara uliokuwa na timu ya awali ya walinzi wa Rais, ikiwa ni pamoja na maajenti wa usalama wa serikali ya DSS, itifaki ya rais na maafisa wa vyombo vya habari.

“Washambuliaji walifyatulia risasi msafara huo baada ya kuuvamia lakini wakazuiwa na wanajeshi, polisi na wafanyakazi wa DSS walioandamana na msafara huo,” ilisema taarifa kutoka ofisi ya Rais.

“Watu wawili kwenye msafara wanapokea matibabu kutokana na majeraha madogo waliyoyapata. Wafanyakazi wengine wote, wafanyakazi na magari walifika salama Daura.”

Haijafahamika mara moja ni nani aliyetekeleza shambulio hilo.

Buhari anajiuzulu mwaka ujao baada ya mihula miwili ya kuwa madarakani huku vikosi vya usalama vya Nigeria vikiendelea kupambana na uasi uliodumu kwa miaka 13 wa wanajihadi kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na magenge ya wahalifu wenye silaha nzito wanaoendesha harakati zao kaskazini magharibi.

Wanamgambo wenye silaha wanaojulikana kienyeji kama majambazi mara nyingi huvamia na kupora vijiji na kutekeleza utekaji nyara wa watu wengi ili kuwakomboa licha ya operesheni za kijeshi dhidi yao kaskazini magharibi na katikati mwa Nigeria.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted