Sri Lanka: Wagombea watatu wateuliwa kuchukua nafasi ya rais wa zamani Gotabaya Rajapaksa

Wagombea watatu waliteuliwa Jumanne kuchukua nafasi ya rais wa zamani wa Sri Lanka Gotabaya Rajapaksa, ambaye alitoroka nchi na kujiuzulu wiki iliyopita

0
Gotabaya Rajapaksa, Rais wa zamani wa Sri Lanka (Photo by Ishara S. KODIKARA / AFP)

Wagombea watatu waliteuliwa Jumanne kuchukua nafasi ya rais wa zamani wa Sri Lanka Gotabaya Rajapaksa, ambaye alitoroka nchi na kujiuzulu wiki iliyopita baada ya waandamanaji kuvamia makazi yake.

Atakayeibuka mshindi atachukua mamlaka ya taifa lililofilisika na ambalo liko kwenye mazungumzo na IMF kwa ajili ya kulinusuru, huku watu wake milioni 22 wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, mafuta na madawa.

Sri Lanka iliishiwa na fedha za kigeni ili kufadhili hata uagizaji wa bidhaa muhimu katika mzozo uliosababishwa na janga la UVIKO 19 lakini uliozidishwa na usimamizi mbaya, wakosoaji wanasema.

Maandamano ya miezi kadhaa yalifikia kilele na kumlazimu Rajapaksa kukimbia makai yake kabla ya kusafiri hadi Maldives na kisha Singapore, ambapo aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu.

Bunge lilitangaza Jumanne kwamba kaimu Rais Ranil Wickremesinghe atapambana na waziri wa zamani wa elimu Dullas Alahapperuma ambaye anaungwa mkono na upinzani mkuu na kiongozi wa mrengo wa kushoto Anura Dissanayake katika kura ya siri siku ya Jumatano.

Watatu hao waliteuliwa rasmi na wabunge katika kikao kilichochukua chini ya dakika 10 katika majengo ya bunge.

Muda mfupi kabla, kiongozi wa chama cha upinzani cha SJB Sajith Premadasa alikuwa ametangaza kwenye Twitter kwamba anajiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho na kumpendekeza Alahapperuma mwenye umri wa miaka 63, mwanachama mpinzani wa chama cha SLPP kilichogawanyika cha Rajapaksa.

Lakini Wickremesinghe, 73, mwanasiasa mkongwe na ambaye amewahi kuwa waziri mkuu mara sita, anaungwa mkono rasmi na uongozi wa SLPP, chama ambacho kinasalia kuwa chama kikuu katika bunge lenye wabunge 225.

Iwapo Wickremesinghe atathibitishwa katika wadhifa huo, anatarajiwa kumtaja waziri wa utawala wa umma Dinesh Gunawardena, rafiki yake wa jadi na mwaminifu mkubwa wa Rajapaksa, kama waziri mkuu mpya.

Mgombea wa tatu ni Anura Dissanayake, 53, kiongozi wa chama cha mrengo wa kushoto cha JVP, au People’s Liberation Front, ambacho kina viti vitatu vya ubunge.

Mgombea wa nne ni mkuu wa zamani wa jeshi Sarath Fonseka, aliyeshindwa kupata uungwaji mkono kutoka kwa wabunge kuingia katika kinyang’anyiro cha urais.

Kiongozi huyo mpya atakuwa ofisini kwa kipindi kilichosalia cha muhula wa Rajapaksa, ambao utaendelea hadi Novemba 2024.

Siku ya Jumatatu, Wickremesinghe aliongeza muda wa hali ya hatari na kutoa mamlaka makubwa kwa polisi na vikosi vya usalama kukabiliana na wasumbufu.

Waandamanaji waliofaulu kumfurusha Rajapaksa walikuwa wakipanga maandamano mengine katika mji mkuu baadaye Jumanne kumtaka Wickremesinghe ajiuzulu.

Wanamwona kama mshirika na mlinzi wa ukoo wa Rajapaksa, ambao umetawala siasa katika nchi hiyo kwa miaka kadhaa.

Rais wa zamani Mahinda Rajapaksa, kaka mkubwa wa Gotabaya aliyeondolewa madarakani na mkuu wa kundi hilo, bado yuko Sri Lanka na vyanzo vya chama vilisema alikuwa akiwashinikiza wabunge wa SLPP kumuunga mkono Wickremesinghe.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted